Korea Kaskazini yarusha kombora la kuvuka mabara
4 Julai 2017Trump amedai China inastahili kusitisha kile alichokiita "ujinga wa Korea Kaskazini" mara moja, huku Urusi ikisema kombora hilo halitoi kitisho chochote kwake. Korea Kaskazini imesema Jumanne, imefanikiwa kulifanyia majaribio kombora lake la kwanza la kutoka bara moja hadi jingine, hiyo ikiwa hatua muhimu katika harakati zake za kutengeneza kombora la nyuklia lenye uwezo wa kuishambulia Marekani.
Wataalam wa Marekani walisema kombora hilo lina uwezo wa kufika Alaska na uzinduzi wake, unaokuja wakati ambapo Wamarekani Jumanne wanaadhimisha siku ya uhuru umemfanya rais Trump kuonesha ghadhabu zake kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter. Umiliki wa Korea Kaskazini wa kombora hilo lenye uwezo wa kwenda umbali wa zaidi ya kilomita 5,500 na pia kutoka bara moja hadi jingine, jambo ambalo Trump aliapa halitofanyika, litaifanya Marekani kupiga hesabu zake upya kuhusiana na kitisho kinachosababishwa na taifa hilo lililotengwa.
China inachunguza uzinduzi wa kombora hilo
Kulingana na mtangazaji katika televisheni ya taifa ya Korea Kaskazini, uzinduzi wa kombora hilo ulishuhudiwa na kiongozi wa nchi hiyo Kim Jong-Un.
Uzinduzi huo ambao maafisa kutoka Korea Kusini walisema ulifanyika katika eneo la Phangyon lililoko mkoa wa Phyongan, unakuja siku chache baada ya Trump kufanya mazungumzo na kiongozi wa Korea Kusini Moon Jae-In katika ikulu ya White House.
Rais Moon wa Korea Kusini kwa upande wake alisema, jeshi la nchi yake linachunguza uzinduzi wa kombora hilo ambalo Urusi kupitia jeshi lake imesema lilikuwa kombora la masafa ya kati.
"Kulingana na maamuzi makuu yaliyofanywa na serikali za Marekani na Korea Kusini, uzinduzi huu unaaminika kuwa uzinduzi wa kombora lenye uwezo wa kuruka umbali wa kadri," alisema Moon, "ingawa tunachunguza uwezekano kwamba kombora hilo lililikuwa lenye uwezo wa kutoka bara moja hadi jengine. Iwapo litakuwa kombora aina hiyo basi tutapata mbinu ya kujibu."
Trump anaisisitizia China kuihimiza Korea Kaskazini kusitisha mipango yake ya nyuklia
Japan nayo kupitia msemaji wa serikali Yoshihide Suga ilisema, kombora hilo lilitua karibu kilomita 300 kutoka rasi ya Oga iliyoko kaskazini magharibi mwa Japan.
"Uzinduzi wa kombora leo ni jambo kubwa sana ukizingatia usalama wa ndege na meli katika eneo hilo pamoja na ukiukaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa. Japan inapinga vikali kwa kuwa hatuwezi kukubali uchokozi wake wa mara kwa mara," alisema Suga. "Tutaendelea kufanya tunaloweza, tukusanye na kuchunguza taarifa, na tutangaze mapya tuliyo nayo karibuni."
Rais Trump amekuwa akiitaka China ambayo ni rafiki wa karibu wa kidiplomasia wa Korea Kaskazini, kuihimiza nchi hiyo kusitisha mipango yake ya nyuklia na makombora na China imejibu ikisema inafanya juhudi kubwa. Gazeti la New York Times limeripoti kwamba, katika mazungumzo ya simu aliyofanya na rais wa China Xi Jinping, rais huyo wa Marekani alisema jeshi la Marekani liko tayari kuchukua hatua dhidi ya Korea Kaskazini.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE/APE
Mhariri: Yusuf Saumu