1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yaitishia Marekani kwa vita vya nuklea

7 Machi 2013

Korea Kusini hapo Alhamisi (07.03.2013) imetishia kufanya shambulio la nuklea la kujihami dhidi ya Marekani na wachokozi wengine wowote wale .

https://p.dw.com/p/17t91
Silaha za Korea Kaskazini
Silaha za Korea KaskaziniPicha: imago/Xinhua

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini pia ameonya kwamba vita vya pili vya Korea haviepukiki kutokana na Marekani na Korea Kusini kuyakataa madai ya Korea Kaskazini ya kufuta mazoezi ya kijeshi ya kiwango kikubwa yaliopangwa kufanywa kwa pamoja na nchi hizo wiki ijayo.Msemaji huyo amesema katika taarifa iliyoonyeshwa hewani na Shirika Kuu la Habari la Korea Kaskazini (KCNA) kwamba kwa kuwa sasa Marekani imejiandaa kuwasha moto wa vita vya nuklea,vikosi vyao vya majeshi ya mapinduzi vitakuwa na haki ya kuanzisha shambulio la nuklea la kujihami kuangamiza ngome kuu za wachokozi.

Wanajeshi wa Marekani wakati wa mafunzo ya kijeshi Korea Kusini (07.03.2013)
Wanajeshi wa Marekani wakati wa mafunzo ya kijeshi Korea Kusini (07.03.2013)Picha: Reuters

Tishio la Korea Kaskazini sio la kwanza

Huko nyuma Korea Kaskazini ilikuwa imetishia kushambulia vikosi vya Marekani vilioko Korea Kusini na pia kudai kuwa inamiliki makombora ya masafa marefu ambayo yana uwezo wa kubeba mabomu ya nuklea na kuifikia Marekani.Tishio hilo linakuja siku mbili baada ya jeshi la Korea Kaskazini kutangaza kwamba itayachanilia mbali mapatano ya kusitisha mapigano ya mwaka 1953 yaliokomesha vita vya Korea hatua ambayo kinadharia itafunguwa njia ya kuanza tena kwa uhasama kati ya nchi hizo.Hali ya wasi wasi imeongezeka mno katika rasi ya Korea hivi karibuni kabla ya kupigwa kura ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mazoezi ya kijeshi ya pamoja kati ya Marekani na Korea Kaskazini yaliopangwa kuanza hapo Jumatatu.

Vikwazo vikali

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Alhamisi(07.03.2013) limeimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini baada ya kuilani nchi hiyo kwa kufanya jaribio la silaha ya nuklea mwezi uliopita.Vikwazo hivyo ni vikali kabisa kuwahi kuidhinishwa na Umoja wa Mataifa ambapo azimio la vikwazo hivyo pia linatishia kuchukuwa hatua zaidi iwapo Korea Kaskazini itafanya jaribio jipya la silaha za nuklea au kurusha roketi.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura kuimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini (07.03.2013).
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakipiga kura kuimarisha vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini (07.03.2013).Picha: picture-alliance/ap

Taarifa ya Alhamisi iliotolewa na wizara ya mambo ya nje imeonya kwamba kupitishwa kwa azimio hilo kutaharakisha mipango ya Korea Kaskazini kutekeleza ahadi zake za kuchukuwa hatua kali za kujibu mapigo.Msemaji wa wizara hiyo pia amesisitiza kwamba uamuzi wa kubatilisha makubaliano ya kusistisha mapigano ya mwaka 1953 kutaanza kufanya kazi wakati mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini yatakapoanza hapo Jumatatu.Amesema hiyo inamaanisha kwamba kuanzia wakati huo vikosi vya majeshi ya mapinduzi vitachukuwa hatua ya kijeshi kwa ajili ya kujihami dhidi ya eneo lolote lile na wakati wowote ule.

Misuli ya kijeshi ya Korea Kaskazini

Wakati huo huo televisheni ya Korea Kaskazini imeonyesha maandamano makubwa ya kijeshi na kiraia yaliofanyika Alhamisi katika uwanja mkubwa kabisa wa Kim Il-Sung mjini Pyongyang.Maandamano hayo yalihutubiwa na maafisa waandamizi wa kijeshi na wa chama ambao wameishutumu Marekani na kuionya serikali ya nchi hiyo kwamba itavuna matokeo iliyopanda ya uchokozi.

Gwaride la kijeshi lililofanyika katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang (15.04.2012).
Gwaride la kijeshi lililofanyika katika mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang (15.04.2012).Picha: imago/Xinhua

Korea Kaskazini inatajwa kuwa bado kabisa iko mbali kuweza kutengeneza bomu la nuklea litakaloweza kurushwa hadi Marekani.Roketi lililorushwa kwa mafanikio hapo mwezi wa Disemba linadokeza kupigwa kwa hatua fulani za maendeleo katika teknolojia ya makombora ya masafa ya marefu lakini yasio na uwezo wa kuvuka mabara.Hii pia sio mara ya kwanza kwa Korea Kaskazini kutishia kuachana na mapatano ya kusitisha mapigano,

ilitowa ahadi kama hiyo hapo mwaka 2009.

Kwa sababu wapiganaji wa Vita vya Korea kamwe hawakuwahi kusaini mkataba wa amani,Korea hizo mbili kitaalamu zinaendelea kuwa vitani ambapo mapatano hayo ya suluhu yanatumika kama mkataba wa kusitisha mapigano.

Mwandishi:Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu