Korea Kaskazini yafyatua makombora ya masafa mafupi
26 Agosti 2017Hayo ni wakati washirika hao wawili, Marekani na Korea Kusini wakifanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya kila mwaka ambayo Korea Kaskazini inayaelezea kuwa ni matayarisho ya vita.
Kituo cha jeshi la Marekani katika ukanda wa Pasifik kimesema kiligundua makombora matatu ya masafa mafupi, yaliyofyatuliwa ndani ya kipindi cha dakika 20. Makombora yote matatu yalifeli, ambapo moja lililipuka maramoja baada ya kufyatuliwa, wakati mengine mawili yalishindwa wakati yakiwa angani.
Ofisi ya Korea Kusini ya Wakuu wa Jeshi imesema majaribio hayo yalifanywa kutokea mkoa wa mashariki wa Korea Kaskazini wa Kangwon na yakaruka katika upande wa kaskazini mashariki karibu kilomita 250 kuelekea baharini.
Kamandi ya Pasifik imesema makombora hayo hayakuweka kitisho chochote kwa ardhi ya Marekani wala katika kisiwa chake cha Guam,a mbacho Korea Kaskazini ilitishia mapema mwezi huu kukizingira "katika bahari ya moto”
Mvutano ulikuwa umepungua tangu majibizano ya maneno makali kati ya Korea Kaskazini na Marekani baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumuonya kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kuwa angekabiliwa na "moto” kama ataitishia Marekani. Ikulu ya White House imesema Rais Trump amefahamishwa kuhusu makombora hayo lakini hajaweza kutoa kauli yoyote.
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani haikuzungumzia maramoja kuhusu majaribio hayo ya Jumamosi. Waziri wa Mambo ya Kigeni Rex Tillerson mapema wiki hii aliipongeza Korea Kaskazini kwa kuonyesha kujizuia kwa kutofyatua makombora tangu jaribio la Kombora la Masafa Marefu lililofanywa mwishoni mwa mwezi Julai.
Tillerson alisema anatumai kuwa kutofyatua makombora au kutofanya "vitendo vingine vya uchochezi” kutoka Korea Kaskazini huenda kukaamanisha barabara huenda ikafungua mazungumzo "katika siku za karibuni”.
Trump pia alielezea matumaini mapema wiki hii kuhusu uwezekano wa kuimarika mahusiano. "naheshimu ukweli kwamba anaanza kutuheshimu,” Trump alisema kumhusu Kim.
Vyombo vya habari vya Korea Kaskazini vimeripoti Jumamosi kuwa Kim aliongoza mazoezi ya jeshi la majini na mashambulizi ya angani.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sudi Mnette