Korea Kaskazini yafyatua kombora kuelekea Japan
4 Oktoba 2022Serikali ya Japan imesema Korea Kaskazini imefyatua kombora hilo kuelekea kwenye kisiwa cha Hokkaido na mkoa wake wa kaskazini mashariki wa Aomori. Waziri anayehusika na kusimamia sera za baraza la mawaziri la Japan, Hirokazu Matsuno amesema kombora hilo limeangukia katika Bahari ya Pasifiki umbali wa kilomita 3,000 kutoka kwenye visiwa hivyo.
Maafisa wa Japan na Korea Kusini wamesema kombora hilo limesafiri umbali wa kilomita 4,500 kwa jumla. Matsuno amesema wamekusanya taarifa kuhusu ndege na meli zilizokuwa zinasafiri kwenye maeneo ya karibu kwa wakati huo, lakini hakuna madhara yoyote yaliyotokea.
Vitendo vya Korea Kaskazini vinatishia usalama wa Japan
''Vitendo vinavyofanywa na Korea Kaskazini, ikiwemo kurusha makombora mara kwa mara vinatishia amani na usalama wa nchi yetu, na jumuia yote ya kimataifa. Aidha, urushaji wa makombora haya kunakiuka Azimio la Baraza la Usalama,'' alifafanua Matsuno.
Maazimio ya Umoja wa Mataifa yanaipiga marufuku Korea Kaskazini kufanya majaribio ya aina yoyote ya makombora. Hata hivyo, hilo ni jaribio la tano kufanywa na Korea Kaskazini ndani ya siku 10. Siku ya Jumamosi Korea Kaskazini ilirusha makombora mawili ya masafa mafupi. Korea Kaskazini imeongeza majaribio ya makombora ikiwa ni katika kujibu luteka ya pamoja ya kijeshi inayofanywa na Korea Kusini na Marekani.
Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida amelaani vikali ufyatuaji huo wa kombora akisema kitendo hicho ni cha kikatili. Kishida amesema nchi yake haijatumia njia zozote za kijeshi kuliharibu kombora hilo ambalo limeruka Japan kutokea Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2017. Hata hivyo, maafisa wa Japan wamewataka wananchi kuondoka katika maeneo ya karibu na tukio hilo.
Rais wa Korea Kusini, Yoon Suk-Yeol ameapa Jumanne kuwa vitendo vya Korea Kaskazini vitajibiwa vikali. Yoon amesema uchokozi wa Korea Kaskazini ni wazi unakiuka misingi na kanuni za Umoja wa Mataifa na ameamuru hatua kali zichukuliwe kwa ushirikiano wa Marekani na jumuia ya kimataifa.
Marekani yalaani, yazungumza na Japan na Korea Kusini
Nalo Baraza la Usalama la Korea Kusini limelaani vikali jaribio hilo la kombora, likisema vitendo vya kichokozi vya Korea Kaskazini haviwezi kuvumiliwa na vitaimarisha ushirikiano wa kiusalama kati yake na Marekani na Japan.
Ikulu ya Marekani imekiita kitendo hicho kuwa cha hatari na kwamba mshauri wa Usalama wa Marekani, Jake Sullivan amewasiliana na wenzake wa Korea Kusini na Japan kuhusu hatua madhubuti za kimataifa za kuchukua. Sullivan amesisitiza nia ya Marekani katika kuzilinda nchi hizo za Asia. Jaribio hilo limelaaniwa pia na mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani katika eneo la Asia Mashariki, Daniel Kritenbrink na Kamandi ya Marekani katika eneo la Indo-Pasifiki. Kritenbrink amesema tukio hilo ni la kusikitisha na ametoa wito wa kufanyika mazungumzo.
(AFP, AP, DPA, Reuters)