Korea Kaskazini yafyatua kombora jengine
15 Septemba 2017Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kutoa ujumbe wa wazi kwa Korea kaskazini kutokana na kitendo hicho cha uchokozi.
Tangu pale rais wa Marekani Donald Trump alipoitishia Korea kaskazini kwa kile alichosema "kutakuwa na moto na hasira" mwezi Agosti, Pyongyang imekwisha fanya jaribio lake kubwa la kinyuklia, ikitishia kurusha makombora katika eneo la maji kuzunguka kisiwa cha Guam na kufanya majaribio ya makombora mawili ambayo yanaruka kwa masafa ya mbali zaidi kupitia anga ya mshirika wa Marekani , Japan.
Ongezeko la wimbi la kurusha makombora, nguvu na kujiamini kunakooneshwa na majaribio haya kunaonekana kuthibitisha kile serikali mbali mbali na wataalamu wa nje walichosema kwa muda mrefu kuwa Korea kaskazini ipo karibu na lengo lake la kujenga hazina ya silaha za kijeshi ambazo zinaweza kulenga majeshi ya Marekani katika eneo la Asia na pia kufika katika ardhi ya Marekani kwenyewe. Kwa upande mwingine , hii ina maana ya kuzusha shaka nchini Korea kusini na Japan kwamba Marekani itahatarisha kusagwasagwa kwa mji wa nchi yake ili kuwalinda washirika wake katika bara la Asia.
Jopo la wakuu wa vikosi vya majeshi ya Korea kusini limesema kombora hilo liliruka kwa kiasi cha umbali wa kilometa 3,700 na kufikia kima cha juu kabisa cha kilometa 770 kwenda juu.
Korea kaskazini imekuwa ikiapa kuendelea na majaribio yake kutokana na kile inachokiita uhasama wa Marekani dhidi yake, ikiwa na maana ya kuwapo kwa mamia kwa maelfu ya wanajeshi wa Marekani nchini Japan na Korea kusini.
Mazungumzo yamekwama
Mazungumzo ya kidiplomasia kuhusiana na suala hilo yamekwama kwa miaka kadhaa, na kuna ishara ndogo kwamba maafisa wa ngazi ya juu kutoka Pyongyang na Washington huenda wakakaa pamoja kujadili njia za kupunguza kasi ya Korea kaskazini yenye dhamira ya kujumuishwa miongoni mwa nchi zenye nguvu za silaha za kinyuklia.Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe amesema.
"Korea kaskazini imekaidi nia ya jumuiya ya kimataifa kufikia suluhisho la amani , na kwamba Japan haitavumilia kitendo kama hicho."
Kombora la leo ambalo, Korea kusini inasema ni la 19 kurushwa na Korea kaskazini mwaka huu , lilisababisha tahadhari ya ving'ora na tahadhari kutolewa kaskazini mwa Japan lakini hakuna uharibifu uliotokea kwa ndege ama meli.
Jaribio hilo limezusha tena matamshi makali. Rais wa Korea kusini Moon Jae-In ameamuru jeshi lake kufanya luteka ya kufyatua makombora ya mwendo wa kasi kujibu hatua ya Korea kaskazini na kuwapa maelekezo maafisa wa serikali kutafakari kuchukua hatua kali ili kuikatisha tamaa Korea kaskazini kuendelea na uchukozi.
Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Jim Mattis wamelieleza jaribio hilo la Korea kaskazini kuwa ni kitendo kilichofanywa bila kuchukua tahadhari. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepanga kikao cha dharura na cha faragha kitakachofanyika leo mchana mjini New York kujadili suala hilo. Jumuiya ya NATO imetaka pachukuliwe hatua na jumuiya ya kimataifa kuhusu jaribio hilo la kombora la Korea ya kaskazini.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape
Mhariri: Iddi Ssessanga