Korea Kaskazini yafanya jaribio lengine la kombora
22 Mei 2017Shirika la habari la serikali ya Korea Kaskazini liliripoti kwamba kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, binafsi alilisimamia jaribio hilo la Jumapili (21.05.2017) ambalo limeibua ukosoaji kutoka kwa jumuiya ya kimataifa na vitisho vya vikwazo vikali zaidi. Shirika hilo lilisema kombora lililofanyiwa majaribio ni aina ya Pukguksong-2 linalotumia nishati na nyenzo zilizoganda zinazoruhusu kuweza kufyetuliwa mara moja na kwa haraka.
Kwa mujibu wa jeshi la Korea Kusini, kombora hilo ambalo lilielezwa na Marekani kuwa la masafa mafupi lilifyetuliwa kutoka Pukchang katika mkoa wa Pyongan Kusini na kusafiri umbali wa kilometa 500 kabla kuanguka katika bahari ya Japan. Msemaji wa mnadhimu wa majeshi ya Korea Kusini aliwaambia waandishi wa habari kwamba maafisa wa ujasusi wa Korea Kusini na Marekani wanatathmini Korea Kaskazini imepata data muhimu kuendeleza uimara wa teknolojia yake ya makombora kupitia jaribio la jana.
Marekani, Korea Kusini na Japan zilililaani vikali jaribio hilo na kwa pamoja zimetaka kikao cha dharura cha baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kulijadili suala hilo, kikao ambacho kitafanyika hapo kesho.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kusini ililikosoa jaribio hilo ikilieleza kuwa hatua ya kutojali na kutowajibika inayoyazima matumaini ya kuziangamiza silaha za nyuklia na kupatikana amani katika rasi ya Korea. Shirika la habari la Yonhap liliripoti kwamba rais Moon Jae-in aliitisha mkutano wa dharura wa baraza lake la usalama wa taifa kulijadili jaribio la kombora la Korea Kaskazini.
Korea Kusini kutathmini upya uhusiano na Korea Kaskazini
Wizara ya Muungano nchini Korea Kusini ilisema itadurusu upya mahusiano yake na Korea Kaskazini. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Seoul, msemaji wa wizara hiyo Lee Deok-haeng alisema hali ya sasa ya mahusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini hairidhishi. "Kulifanyika jaribio la kombora jana na serikali mpya ya rais mpya wa Korea Kusini Moon Jae-in itachukua hatua kali kufuatia uchokozi wa Korea Kaskaini. Uhusiano kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini umevurugika na unaiyumbisha rasi ya Korea. Tutauangalia tena uhusiano wetu pasi na kuvikwamisha vikwazo vya jumuiya ya kimataifa dhidi ya Korea Kaskazini."
Serikali ya Japan ilisema imejizatiti kuweka vikwazo vyake yenyewe kuzuia azma ya Korea Kaskazini kuwa na silaha za nyuklia huku ikiendelea kuhakikisha vikwazo vya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa vitatekelezwa kikamilifu. Msemaji wa serikali Yoshihide Suga alisema kuzuia fedha, vifaa na teknolojia ambayo Korea Kaskazini inaihitaji kwa mpango wake wa nyuklia ni muhimu katika kuukwamisha mpango mzima wa nyuklia wa taifa hilo.
"Hatuwezi kukubali Korea Kaskazini iendelee na tabia yake ya uchokozi. Ili kuuzuia mpango wake wa nyuklia na makombora, tunaamini ni muhimu kuzuia fedha za kigeni na meli za mizigo pamoja na usafirishaji wa teknolojia inayohusiana na uendelezaji na utengenezaji wa silaza na nyuklia."
Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, alisema jaribio la kombora ni dharau na changamoto kwa jitihada za jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhisho la amani.
Jaribio hilo lilifanywa wiki moja tu baada ya Korea Kaskazini kulifanyia jaribio kombora la masafa marefu aina ya Hwasong-12, ambalo kwa mujibu wa Pyongyang lina uwezo wa kubeba kichwa 'kizito' cha nyuklia.
Mwandishi:Josephat Charo/afpe/ape
Mhariri:Iddi Sessanga