1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

N.Korea test

Halima Nyanza25 Mei 2009

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana leo kwa dharura kujadili jaribio la nyuklia la Korea kaskazini. Mapema leo Korea kaskazini ilitangaza kuwa imefanikiwa kufanya jaribio jengine la kombora la nyuklia.

https://p.dw.com/p/HwqR
Picha inaonesha Kombora la Korea kaskazini likifyatuliwa katika eneo la Musudan-ri. Korea kaskazini leo imesema imefanya tena jaribio lake la nyuklia kwa mafanikio.Picha: AP

Mara tu baada ya Korea kaskazini kutangaza kuwa imefanikiwa kufanyaa jaribio lake la nyuklia, hatua ambayo inatoa uhakika wa kutengwa kwa taifa hilo, ambalo limesema halina uamuzi mwingine, ila kujenga ghala la silaha za nyuklia kwa ajili ya kujilinda yenyewe na maadui zake duniani, hali ya wasiwasi imejitokeza na kauli mbali zimetolewa.


Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin amearifu kuwa Baraza la Usalama la Umoja huo litakutana leo kujadili uamuzi huo wa Korea kaskazini.


Aidha maafisa wa Urusi wamesema wanafanyia uchunguzi ripoti zilizotolewa na Korea kaskazini kuhusiana na jaribio hilo.


Huku Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo ikisema nguvu ya mlipuko huo wa nyuklia ulikuwa kati ya kilo tani 10 na 20.


kukadiriwa kwa nguvu hiyo iliyotumika, kunafanya jaribio hilo la leo kuwa na nguvu zaidi kushinda lile Korea Kaskazini iliyofanya kwa mara ya kwanza mwaka 2006, pia karibu na mji wa Kilju ambalo limeelezwa kuwa chini zaidi ya kilo tani moja.


Jaribio la leo, ambalo ni la pili kufanywa na Korea kaskazini linafuatia miaka kadhaa ya majadiliano kulishinikiza taifa hilo masikini kuachana na mpango wake huo wa kuendelea na mradi wake wa nyuklia.


Aidha Ikichochea wasiwasi zaidi, Korea Kaskazini imerusha kombora lake la masafa mafupi muda mchache tu baada ya kusema kuwa imefanikiwa kuendesha jaribio hilo la nyuklia.


Aidha habari za kuendesha kwa jaribio hilo la Nyuklia, zimeyumbisha masoko ya fedha ya Korea kusini, hususan kwa kwa hofu kwamba jaribio hilo litaongeza wasiwasi katika eneo hilo lenye nguvu kiuchumi duniani.


Bei za hisa zimeripotiwa kupungua kwa asilimia nne katika soko la fedha mjini Seol kutokana na hali ya wasiwasi iliyozuka katika kanda hiyo.


Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Korea Kaskazini jaribio hilo la chini ya ardhi limeendeshwa bila ya wasiwasi na katika kiwango cha juu kipya.


Lakini hata hivyo itachukua muda kabla ya nchi nyingine duniani kuweza kupima mafanikio yake.


Tayari viongozi mbalimbali duniani wamelaani jaribio hilo, ambapo Rais Barack Obama amesema majaribio hayo ya nyuklia na makombora yanatishia amani ya kimataifa na kutaka kuchukuliwa hatua na jumuia ya kimataifa.


Aidha Marekani nayo imesema imekuwa ikijadiliana na washirika wao pamoja na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya hatua itakayofuata baada ya kutangazwa kuendeshwa kwa jaribio hilo.


Kwa upande wake, Japan imesema jaribio hilo halikubaliki na kwamba linakiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.


Nayo Uingereza imesema pia tangazo hilo la Korea kaskazini ni wazi limevunja azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuitaka nchi hiyo kurejea tena katika mazungumzo ya pande sita, kuachana na mpango wake huo.


Naye Kamishna wa Masuala ya Nje wa Umoja wa Ulaya Benita Ferrero Waldner amesema jaribio hilo linapaswa kushutumiwa kutokana na kusababisha wasiwasi mkubwa, huku Korea kusini ikisema jaribio hilo linahatarisha amani ya dunia.


Mwandishi: Halima Nyanza (AFP/AP/Reuters)

Mhariri: M.Abdul-Rahman