1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini yafanya jaribio la bomu la nyuklia

9 Septemba 2016

Marekani na Urusi zimesema zitalifikisha suala la jaribio la bomu la nyuklia lilofanywa na Korea Kaskazini kwa Umoja wa Mataifa baada ya nchi hiyo kufanya jaribio hilo Ijumaa (09.09.2016) na kushutumiwa duniani kote.

https://p.dw.com/p/1Jz2d
Picha: picture-alliance/dpa/Kcna

Tangazo la taifa la Korea Kaskazini limesema leo hii wanasayansi wao na mafundi wa Taasisi ya Majaribio ya Silaha za Nyuklia wamefanya jaribio la kuripua bomu la nyuklia katika eneo la kaskazini la kufanyia majaribio hayo kuona nguvu ya bomu hilo jipya lililotengenezwa hivi karibuni na hakuna vitu vya sumu vilivyovuja kwa hiyo hakuna madhara ya ekolojia na mazingira katika eneo husika.

Imesema imefanya jaribio lake la tano la silaha za nyuklia masaa machache baada wataalamu wa matetemeko ya ardhi kugunduwa mripuko karibu na eneo la siri linalotumiwa na nchi hiyo kufanyia majaribio ya silaha za nyuklia.

Televisheni hiyo ya taifa ya Korea Kaskazini imesema nchi hiyo hivi sasa ina uwezo wa kurusha mabomu ya nyuklia kwa kutumia maroketi ya masafa marefu.

Jaribio ndio kubwa kabisa

Tetemeko la ardhi lenye guvu ya kipimo cha 5.3 lililotokea kama matokeo ya jaribio hilo limeonyesha mripuko huo ulikuwa na uzito wa kilotoni 10 na ni kubwa kabisa kuwahi kufanywa na nchi hiyo.

Korea Kaskazini ikitowa tangazo lake la jaribio la bomu la nyuklia .
Korea Kaskazini ikitowa tangazo lake la jaribio la bomu la nyuklia .Picha: Reuters/KRT

Tetemeko hilo limegunduliwa karibu na eneo la kufanyia majaribio ya silaha za nyuklia nchini humo la Punggye- ri wakati nchi hiyo ikiadhimisha Siku ya Kuasisiwa kwa taifa hilo mwaka1948.

Tangazo hilo limekuja sio muda mrefu baada ya Rais wa Korea Kusini Park Geun -hye kumshambulia kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Ung kwa hatua yake aliyoita ya wenda wazimu.

Jaribio lalaaniwa

Waziri Mkuu wa Korea Kusini Hwang Kyo- anh ameitisha kikao cha baraza la usalama wa taifa kujadili jaribio hilo la tano la bomu la nyuklia la Korea Kaskazini.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov.Picha: picture-alliance/dpa/A.Shcherbak

Hwang amesema "Jaribio hili la bomu la nyuklia ambalo limefanyika licha ya nchi hiyo kuwa chini ya vikwazo vikubwa ambavyo iliwekewa baada ya kufanya jaribio lake la nne la bomu la nyuklia ni wazi kwamba linakwenda kinyume na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ni changamoto dhidi ya jumuiya ya kimataifa.Korea Kusini na jumuiya ya kimataifa inalaani vikali kitendo hicho cha uchokozi cha Korea Kaskazini."

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov wamelaani jaribio hilo leo hii na wamesema kwamba watalifikisha suala hilo kwa Umoja wa Mataifa.

Wamesema wanajaribu kufuatilia na kujuwa nini hasa kilichotokea na kwamba kwa hakika watalijadili jambo hilo Umoja wa Mataifa.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Yusuf Saumu