Korea kaskazini yaendelea na ukaidi yafyatua kombora jingine
29 Aprili 2017Jaribio hilo lililofanywa katika eneo kaskazini mwa mji mkuu wa Korea kaskazini , Pyongyang, linaonekana kuwa limeshindwa, maafisa wa Marekani na Korea kusini wamesema, katika kile ambacho ni jaribio la nne mfululizo la Korea kaskazini kushindwa tangu mwezi Machi.
Jaribio hilo linakuja wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amelionya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba kushindwa kuudhibiti mpango wa kinyuklia na makombora wa Korea kaskazini kunaweza kusababisha "matokeo mabaya".
Maafisa wa Marekani , wakizungumza kwa masharti ya kutotajwa majina, wamesema kombora hilo huenda ni la masafa ya kati linalofahamika kama KN-17 na linaonekana kuwa liliripuka na kuvunjika katika muda wa dakika chache tangu pale lilipofyatuliwa.
Korea kusini imesema nchi hiyo ya kaskazini inacheza na moto na kuionya kwamba itakabiliwa na vikwazo vikali zaidi ya Umoja wa Mataifa.
Ukiukaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa
Jeshi la Korea kusini limesema kwamba kombora hilo , lililofyatuliwa kutoka katika jimbo la Pukchang katika mwelekeo wa kaskazini mashariki, lilifikia umbali hewani wa kilometa 71 kabla ya kuvunjika vunjika dakika chache wakati likiruka. Limesema kurushwa kwa kombora hilo ni ukiukaji wa wazi wa maazimio ya Umoja wa Mataifa na kuionya Korea kaskazini kutochukua hatua bila kufikiria.
Utawala wa rais wa Marekani Donald Trump unaweza kuchukua hatua dhidi ya jaribio hilo la kombora la Korea kaskazini kwa kuharakisha mipango yake kwa ajili ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Pyongyang, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa hatua dhidi ya maeneo mahususi ya Korea kaskazini na China, afisa wa Marekani ameliambia shirika la habari la Reuters jana.
Wakati Korea kaskazini inachukua hatua kwa kukaidi mbinyo kutoka Marekani na mshirika wake mkubwa China, Marekani inaweza kufanya luteka mpya ya jeshi la majini na kuweka meli zaidi za kijeshi na ndege katika eneo hilo kwa nia ya kuonesha uwezo wa nguvu zake , afisa huyo amesema , kwa masharti ya kutotajwa jina.
Vikwazo vipya
Afisa huyo amesema vikwazo vyovyote vipya vinaweza kuwekwa katika siku chache zijazo na vinaweza kulenga idadi kadhaa ya maeneo ambayo tayari yametathminiwa na serikali ya Marekani kwa ajili ya hatua kama hizo, wakati utawala huo wa Marekani unaendelea kutayarisha mpango mkubwa zaidi wa vikwazo.
Maeneo lengwa ya vikwazo hivyo , afisa huyo amesema , yanaweza kuwa taasisi za kifedha na makampuni muhimu ya Korea kaskazini pamoja na China, hatua ambayo huenda ikaikasirisha China.
Wakati rais Trump amemsifu rais wa China Xi Jinping kwa kuashiria ongezeko la ushirikiano kuhusiana na suala la Korea kaskazini , afisa huyo amesema Beijing bado "inahitajika kuchora aina fulani ya msitari mchangani" na Pyongyang kuhusiana na mpango wake wa kinyuklia.
Hatua za kijeshi chini ya hatua zinazofanyiwa tathmini ni pamoja na kuonesha uwezo wa nguvu za Marekani katika eneo hilo zenye lengo la kuizuwia Korea kaskazini na kuihakikishia Korea kusini mshirika mkubwa wa Marekani kuhusu usalama wake, ameeleza afisa huyo wa Marekani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Idd Ssessanga