Korea Kaskazini yaapa kujibu hatua za kijeshi za Marekani
11 Aprili 2017Korea Kaskazini inayachukulia mazoezi hayo ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea Kusini kama matayarisho ya uvamizi huku pia hatua ya hivi karibuni ya Korea Kaskazini kufyatua kombora inakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Korea Kaskazini alikaririwa na shirika la habari la serikali ya nchi hiyo akisema Marekani itawajibika kutokana na vitendo vyake vyoyote vya uchokozi.
Kauli ya Korea Kaskazini inakuja baada ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson kusema mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya kambi ya anga ya Syria ambayo ni hatua ya kulipiza kisasi kufuatia shambulizi la gesi ya sumu ni onyo kwa nchi yoyote inayokwenda kinyume na maadili ya kimataifa.
Ingawa hakuitaja moja kwa moja Korea Kaskazini lakini matamshi ya Tillerson yalionekana zaidi kuilenga Korea Kaskazini ambapo alisema yeyote anayeonekana kuwa kitisho kwa wengine inabidi adhibitiwe pindi inapolazimu kufanya hivyo.
Korea Kaskazini yadai Marekani inajiaandaa na uchukozi dhidi yake
Korea Kaskazini kwa muda mrefu imekuwa ikidai kuwa Marekani imekuwa ikijiandaa kufanya vitendo vya uchokozi dhidi yake na kuwa silaha zake za nyuklia ni njia moja wapo ya kujilinda dhidi ya vitendo hivyo vya uchukozi.
Taarifa ya Korea Kaskazini imekwenda mbali zaidi na kusema kuwa hatua ya Marekani ya kutaka kuivamia Jamhuri ya Korea imefikia kiwango cha juu na kuwa Korea Kaskazini iko tayari kujibu hatua zozote za kijeshi zitakazochukuliwa na Marekani.
Mkazi mmoja wa Korea Kaskazini Kim Song Chul ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa wananchi wa taifa hilo wanapenda amani lakini kamwe hawataiomba na iwapo mtu yeyote atajaribu kuwachokoza watajilinda kwa nguvu kubwa na kuwa wataendelea kufanya vile wanavyotaka.
Ni jambo la kawaida kwa meli za kivita za Marekani kuwepo katika ukanda wa Korea na Jumamosi iliyopita wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema wanajeshi wake wa majini walikuwa wakielekea katika bahari ya Pasifiki ili kudhihirisha uwepo wake katika eneo hilo.
Mshauri wa masuala ya usalama wa Rais Donald Trump, H.R. McMaster aliuelezea uamuzi wa kupeleka wanajeshi wa majini katika eneo hilo kama hatua za tahadhari.
Mwandishi: Isaac Gamba/ APE
Mhariri: Iddi Ssessanga