1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini na Kusini zakutana kutuliza mvutano

22 Agosti 2015

Maafisa wakuu wa Korea Kusini na Kaskazini wamekuwa na mazungumzo Jumamosi (22.08.2015) katika kijiji cha amani cha mpakani cha Panmunjom na kuamsha matumaini ya kumaliza mzozo ulioziweka nchi hizo kwenye ukingo wa vita

https://p.dw.com/p/1GJwF
Washauri wakuu wa viongozi wa Korea Kaskazini na Kusini katika mkutano wao wa 22.08.2015.
Washauri wakuu wa viongozi wa Korea Kaskazini na Kusini katika mkutano wao wa 22.08.2015.Picha: Reuters/the Unification Ministry/Yonhap

Mkutano huo katika kijiji hicho kilioko eneo lililopigwa marufuku shuguli za kijeshi yalianza mara tu baada ya kumalizika kwa muda wa mwisho na Korea Kaskazini kuitaka Korea Kusini isitishe matangazo yake ya propaganda kwa kutumia vipaza sauti mpakani venginevyo ingeishambulia kijeshi.

Muda huo umemalizika bila ya kurepotiwa kwa matukio yoyote yale ya vurugu.Kwa mujibu wa wizara ya masuala ya muungano ya Korea Kusini mazungumzo hayo yaliendelea baada ya mkutano wa takriban masaa matatu.

Mashambuliano ya mizinga hapo Alhamisi yamepelekea kutolewa kwa wito wa utulivu na Umoja wa Mataifa, Marekani na China mshirika mkuu pekee wa Korea Kaskazini.Jeshi la Korea Kusini limeendelea kuwa katika hali ya tahadhari licha ya kufanyika kwa mazungumzo hayo.

Haja ya kukutana

Mshauri wa usalama wa taifa wa Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye ambaye pia ni waziri wa masuala ya muungano wa nchi hiyo amekutana na mshauri mkuu wa kijeshi wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong -Un na afisa mkongwe wa serikali katika masuala ya Korea mbili Yang Gon.

Mwanajeshi wa Korea Kusini akiondowa vipaza sauti vya mpakani.
Mwanajeshi wa Korea Kusini akiondowa vipaza sauti vya mpakani.Picha: picture-alliance/dpa/J.H. Park

Awali akizungumza kwa muhtasari katika televisheni Kim Kyou -hyun ambaye ni naibu mshauri wa usalama wa taifa amesema nchi hizo mbili zimekubaliana kuwa na mawasiliano kuhusu hali ilioko sasa katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

Serikali ya Korea Kaskazini awali ilitowa pendekezo hapo Ijumaa kufanyika kwa mkutano huo na serikali ya Korea Kusini ilirudia pendekezo hilo Jumamosi na kutaka ushiriki wa Hwang.

Shirika la habari la serikali Korea Kaskazini KNCA pia lilitangaza mkutano huo na kuitaja Korea Kusini kwa jina la Jamhuri ya Korea jambo la nadra kuitambuwa rasmi hasimu wake huyo kinyume na majigambo ya shari iliokuwa ikiyatowa hivi karibuni.

Kuepuka tahayuri

James Kim mtafiti katika Taasisi ya Masomo ya Sera ya Asan mjini Seoul anasema nchi hizo zinahitajiwa kuwa na makubaliano fulani ambapo nchi zote mbili zitaondokana na tahayuri.

Wanajeshi wa Korea Kusini na wenzao wa Marekani katika mazoezi ya pamoja.
Wanajeshi wa Korea Kusini na wenzao wa Marekani katika mazoezi ya pamoja.Picha: picture-alliance/dpa/Marine Corps

Korea Kaskazini kiufundi bado iko katika vita na Korea Kusini baada ya mzozo wa mwaka 1950-1953 kumalizikia na suluhu na sio mkataba wa amani.

Korea Kusini ilianza kurusha matangazo ya propanda kwa vipaza sauti vikuu hapo tarehe 10 Augusti katika eneo lililopigwa marufuku shughuli za kijeshi baada miripuko ya mabomu katika eneo hili kuwajeruhi wanajeshi wawili wa Korea Kusini.

Korea ya Kaskazini imekanusha kutega mabomu hayo.

Korea Kusini iimesema itaendelea na matangazo hayo venginevyo Korea Kusini ikubali kuwajibika na miripuko hiyo.

Uhusiano kati ya Korea Kaskazini na Kusini ulisitishwa kabisa hapo mwaka 2010 kufuatia kuzamishwa kwa manowari ya Korea Kusini ambapo Korea Kaskazini imekanusha kuhusika kwa njia yoyote ile na tukio hilo.

Mwandishi : Mohamed Dahman /Reuters

Mhariri : Isaac Gamba