Korea Kaskazini kuyagomea mazungumzo ya mataifa sita
14 Aprili 2009Korea Kaskazini imepuuzilia mbali hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kulaani hatua ya kutuma roketi lake katika anga za juu. Huku Marekani na Korea Kusini zikiipongeza hatua hiyo ya baraza la usalama Korea kaskazini inasema itayagomea mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Korea Kaskazini inasema itayagomea mazungumzo ya mataifa sita kupinga taarifa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa inayolaani hatua yake ya kurusha roketi angani. Wizara ya mashauri ya kigeni ya Korea Kaskazini imenukuliwa ikisema kwamba mazungumzo hayo hayana maana yoyote na kwamba inapanga kuanzisha tena shughuli katika vinu vyake vya nyuklia ambavyo vilikuwa vimefungwa.
Urusi imesikitishwa na uamuzi wa Korea Kaskazini kuanzisha tena mpango wake ya nyuklia na kuitaka isijiondoe kwenye meza ya mazungumzo. Japan kwa upande wake imeitaka Korea Kaskazini ikubali taarifa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kuitaka ianzishe tena mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia yaliyokwama.
Siku nane baada ya Korea Kaskazini kurusha roketi lake, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa pamoja limeilaani hatua hiyo, likitaka majaribio ya makombora yakome. Baraza hilo pia limesema litapanua vikwazo dhidi ya taifa hilo la kikomunisti.
Taarifa iliyokubaliwa na nchi zote 15 wanachama wa baraza hilo siku ya Jumatatu inasema jaribio la roketi la Korea Kaskazini linakiuka azimio nambari 1718 lililoidhinishwa mnamo mwaka 2006 baada ya nchi hiyo kufanya majaribio ya silaha za nyuklia.
Marekani imeridhika
Taarifa hiyo ya baraza la usalama ni tamko dhaifu kuliko azimio lililotakiwa na Japan na Marekani lakini lililopingwa na China na Urusi. Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice, amesema Marekani imefurahia uamuzi wa baraza la usalama
"Marekani imefurahi kwamba baraza la usalama leo limetoa taarifa nzito ya pamoja inayolaani wazi jaribio la roketi la Aprili 5 kwamba ni hatua inayokiuka azimio nambari 1718 la baraza la usalama. Na pia kuweka wazi kwamba majaribio yoyote ya siku za usoni yatakuwa pia yanakiuka maazimio yaliyopo ya baraza la usalama."
Susan Rice amesema taarifa hiyo ina mafungamano ya kisheria kama azimio, wazo ambalo linaungwa mkono na Urusi lakini linalopingwa na wanadiplomasia wengine.
Rais wa Marekani, Barack Obama, amesema hatua ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini ni ujumbe wa umoja. Msemaji wa ikulu ya white house mjini Washington, Robert Gibbs, ametoa taarifa akisema rais Obama ameukaribisha ujumbe wa baraza la usalama kwamba hatua ya Korea Kaskazini ni uhalifu na itasababisha athari halisi.
Gibbs amesema jumuiya ya kimataifa imeungana kuishinikiza Korea Kaskazini iachane na juhudi za kutengeza silaha za maangamizi makubwa, usafirishaji wa silaha hizo na iachane na vitendo vya uchokozi.
Mazungumzo kuendelea
Marekani imesema itaendelea kushirikiana na washirika wake katika mazungumzo ya pande sita kufikia lengo la kuangamiza mpango wa silaha za nyuklia za Korea Kaskazini na kupunguza hali ya wasiwasi katika eneo zima la Korea.
China imesisitiza umuhimu wa kuendelea na mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini. Ilikuwa na wasiwasi kwamba tamko la baraza la usalama lingeisababisha Korea Kaskazini kujiondoa kwenye mazungumzo ya mataifa sita.
Akizungumza juu ya taarifa ya baraza la usalama balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Zhang Yesui anasema, "Msimamo wetu kuhusu tamko la baraza la usalama umekuwa wazi kabisa na thabiti. Tamko la baraza la usalama linatakiwa liwe na uangalifu na uwiano na pia lisaidie kuendelea kudumisha amani na uthabiti. Lisaidie pia mazungumzo ya mataifa sita na mchakato wa kuangamiza silaha za nyuklia."
Msimamo wa Korea Kusini
Korea Kusini imesema taarifa ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa ni ujumbe mkali kwa Korea Kaskazini. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kusini, Moon Tae-Young amesema serikali inakaribisha na kuunga mkono tamko hilo. Ameongeza kusema kuwa Korea Kaskazini italazimika kutambua kuwa jumuiya ya kimataifa imetoa kauli kali kupitia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na iachane na vitendo vya uchokozi vinavyohujumu amani na uthabiti katika eneo zima la Korea na kaskazini mashariki mwa Asia.
Ofisi ya rais wa Korea Kusini mjini Seoul imeieleza taarifa ya baraza la usalama kuwa ujumbe ulio wazi na wa umoja. Msemaji wa ofisi hiyo, Lee Dong-Kwan amesema, "Tuna matumaini Korea Kaskazini haitajaribu tena kulifuatilia swala hili kimkakati lakini kwa uangalifu mkubwa itafikiria upya maana ya ujumbe huu na kuwa mwanachama aliyekomaa wa jumuiya ya kimataifa."
Mwandishi: Charo, Josephat/ RTRE
Mhariri: Saumu Mwasimba