1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini, Kusini zakutana

Mohammed Khelef15 Oktoba 2014

Korea ya Kusini na Kaskazini zimefanya mkutano wao wa kwanza wa ngazi za juu wa kijeshi baada ya miaka saba, siku chache baada vikosi vyao kurushiana risasi za kuonyana kwenye mipaka.

https://p.dw.com/p/1DVn8
Meli ya upelelezi ya Korea ya Kusini karibu na mpaka wa baharini na Korea ya Kaskazini.
Meli ya upelelezi ya Korea ya Kusini karibu na mpaka wa baharini na Korea ya Kaskazini.Picha: Reuters/South Korean Coast Guard/Yonhap

Kwa mujibu wa shirika la habari la Yonhap, mazungumzo hayo yaliyojumuisha majenerali wa kijeshi kutoka pande zote mbili yamefanyika kwenye kijiji cha mpakani cha Panmunjom. Mara ya mwisho, mkutano wa ngazi hiyo ulifanyika Disemba 2007.

Inaripotiwa kwamba mkutano huu wa leo umelenga kupunguza uhasama kati yao, baada ya matukio ya kuchokozana wiki iliyopita. Hapo Ijumaa, Korea hizo mbili zilirushiana risasi mpakani baada ya upande wa Kaskazini kujaribu kuyadungua maputo yaliyorushwa kutoka Kusini na wanaharakati wanaoipinga serikali ya Korea ya Kaskazini na Jumanne boti za doria za nchi hizo mbili zikarushiana risasi za onyo karibu na mpaka wa bahari unaozozaniwa.

Baada ya mtafaruku huo, Korea ya Kusini ilisema ingelijibu uchokozi mwengine wowote wa Kaskazini kwa hatua kali za kijeshi, ingawa ilisisitiza kwamba mlango wa majadiliano bado ulikuwa wazi.

Mzozo wa vipeperushi

Mazungumzo ya leo yanahusu hasa namna ya kuutatua mzozo wa mpaka wa baharini, eneo ambalo limekuwa chanzo cha makabiliano kadhaa yaliyosababisha vifo kwa pande zote mbili.

Kikosi cha Korea ya Kaskazini katika moja ya magwaride ya maadhimisho ya Chama cha Wafanyakazi.
Kikosi cha Korea ya Kaskazini katika moja ya magwaride ya maadhimisho ya Chama cha Wafanyakazi.Picha: picture-alliance/dpa/Kyodo

Urushwaji wa vipeperushi vya propaganda unatazamiwa pia kuwa ajenda ya mazungumzo hayo, kwa mujibu wa shirika la habari la Yonhap, likiwanukuu maafisa wa serikali ya Korea ya Kusini.

Korea ya Kaskazini imeitolea wito Kusini kutoruhusu ardhi yake kutumiwa kwa vitendo hivyo inavyoviita vya kiadui, ikiwa kweli inataka mahusiano yao yaimarike, wito ambao Korea ya Kusini inaukaidi ikisema ni suala la uhuru wa kujieleza.

Hata hivyo, shirika la habari la Yonhap linasema Korea ya Kaskazini imeiomba Kusini isiutangaze mkutano huu wa leo kwa sababu za kisiasa. Wizara za Ulinzi na ya Muungano za Korea ya Kusini zimekataa kuthibitisha chochote.

Mkutano huu unafanyika chini ya wiki mbili baada ya maafisa wa ngazi za juu wa Pyongyang kufanya ziara ya kushitukiza nchini Korea ya Kusini kukutana na wenzao wa Seoul, ambayo ilipelekea kufikiwa makubaliano ya mazungumzo mengine ya kidiplomasia mwezi Novemba.

Kwa kuwa mgogoro wa mwaka 1950 hadi 53 ulimalizika kwa tangazo tu la kusitisha mapigano na sio mkataba baina yao, nchi hizo mbili zinatambua kuwa kimsingi bado ziko kwenye vita.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AP
Mhariri: Iddi Ssessanga