Korea Kaskazini kushawishi msimamo wa dunia kuhusu Iran?
6 Aprili 2013Wataalamu wanasema mataifa yenye uwezo mkubwa duniani sasa yana shauku ya kuona kuwa hali wanayoishuhudia Korea Kaskazini haitokei kwa Iran. Siku ya Ijumaa Iran na mataifa matano ya madola ambayo ni wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani walikutana mjini Almaty nchini Kazakhstan kwa mazungumzo mapya ya kutafuta muafaka kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Mtaalamu Mark Fitzpatrick wa taasisi ya kimataifa ya mafunzo ya mikakati anasema nchi hizo za madola zitakuwa zingativu hata zaidi kutafuta suluhu kabla ya kufikia hatua ya Korea Kaskazini na kuwa na silaha za kinyuklia kwani hali Iran itakuwa hatari na mbaya zaidi.
Huku Korea Kaskazini ikiwa tayari imeudhihirishia ulimwengu uwezo wake wa kinyuklia kwa kufanya majaribio mara tatu ikiwemo hivi karibuni mwezi Februari, mjadala kuhusu Iran bado unazunguka iwapo inaunda bomu la kinyuklia kwa kujificha chini ya madai ya mpango wa kusaidia maendeleo ya raia wake.
Iran shingo ngumu licha ya vikwazo
Mataifa ya magharibi yamekuwa yakiishinikiza Iran kupunguza urutubishaji wa madini ya Urani na kufunga kiwanda cha nyuklia cha Fordo, ili kuondolea mbali hofu ya kuwa inatengeza bomu la nyuklia. Iran imekanusha vikali madai hayo lakini juhudi zake za kurutubisha madini ya Urani kwa kiwango kinachoweza kutengeza bomu imesababisha kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa na mataifa ya kigeni ambayo imeathiri taifa hilo vibaya.
Oliver Meier wa taasisi ya kimataifa ya masuala ya usalama ya Ujerumani anasema hata wakati nchi za magharibi zinatafuta kuidhibiti Iran, kutokuwepo kwa matokeo ya matumizi ya nyuklia kutoka Korea Kaskazini kufikia sasa huenda kukaishawishi Iran kuchelewesha au kusitisha juhudi zake za mpango wa nyuklia. Korea Kaskazini imeathirika kutokana na vikwazo ilivyowekewa na Umoja wa Mataifa, imetengwa na mataifa mengine na uchumi wake umedorora.
Iran yafuatilia kwa makini mzozo wa Korea kaskazini
Wakati huo huo mzozo wa sasa wa Korea Kaskazini huenda ukaifunza Iran mambo mawili matatu - inaweza kwenda umbali gani kukiuka shinikizo za magharibi na kwamba Iran inafuatilia kwa makini hali ilivyo Korea kuona ni kwa kiasi gani shinikizo zinaweza kuiathiri.
Kuna tofauti kubwa kati ya Iran na Korea Kaskazini kwani Iran bado inasalia kuwa chini ya mkataba iliyotia saini wa udhibiti wa matumizi ya nyuklia na hivyo kuweza kufanyiwa uchunguzi na shirika la nishati ya Atomic la Umoja wa mataifa, huku Korea Kaskazini ikiwa haishurutishwi na hilo kwani sio mwanachama. Meier anasema ndiyo maana ni muhimu kwa Jumiya ya kimataifa kutoa ujumbe wa wazi kwa Iran kuwa na silaha za nyuklia ni jambo lisilokubalika kamwe.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga.