1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Korea Kaskazini kufungua tena kiwanda cha nyuklia

2 Aprili 2013

Korea Kaskazini imesema kuwa inakusudia kuanzisha upya shughuli katika vinu vyote vya nyuklia kwenye kiwanda chake cha nyuklia katika eneo la Yongbyon, hatua inayochukuliwa ya kiuchokozi kutokana na vitisho inavyovitoa.

https://p.dw.com/p/187wB
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-unPicha: Reuters

Korea Kaskazini imesema kuwa inakusudia kuanzisha upya shughuli katika vinu vyote vya nyuklia kwenye kiwanda chake cha nyuklia katika eneo la Yongbyon, hatua inayochukuliwa kama ya kiuchokozi kutokana na mfululizo wa vitisho vinavyotolewa na nchi hiyo.

Shirika la habari la Korea Kaskazini la KCNA, limesema leo kuwa kufufuliwa kwa shughuli katika kiwanda hicho, kutaongeza utengenezaji wa nyuklia kwa matumizi ya umeme na kijeshi. Kiwanda hicho kilifungwa mwaka 2007 kama sehemu ya mpango wa kimataifa wa kupunguza utengenezaji wa silaha za nyuklia. Tangazo hilo limetolewa wakati ambapo Korea Kusini na Marekani zinaendelea kuviangalia kwa makini vitisho vya Korea Kaskazini wakati wasiwasi kuhusu mzozo kwenye Rasi ya Korea ukizidi kuongezeka.

Rais wa Korea Kusini, Park Geun-Hye
Rais wa Korea Kusini, Park Geun-HyePicha: Getty Images

Hatua hiyo ya Korea Kaskazini inaonekana kama uchokozi wakati ambapo mvutano wa kijeshi ukipamba moto na uamuzi wa Marekani kupeleka ndege za kivita kwenye pwani ya Korea Kusini. Msemaji wa serikali ya Korea Kaskazini anayeshughulikia masuala ya nyuklia, amenukuliwa na KCNA, akisema kuwa shughuli katika kiwanda hicho zitajumuisha kuvifungua tena vinu vyote vya nyuklia, ukiwemo mtambo wa kurutubisha madini ya uraniumu na mtambo wa megawati tano.

Korea Kaskazini ina vifaa vya kuweza kujenga vinu vinane

Inakadiriwa kuwa Korea Kaskazini ina vifaa vya kuweza kujenga hadi vinu vinane vya kutengeneza silaha za nyuklia, ingawa makadirio hayo yanatofautiana. Kwa mujibu wa takwimu iliyotolewa mwaka uliopita wa 2012 na Taasisi ya Sayansi na Usalama wa Kimataifa, Korea Kaskazini ina uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia 21 hadi 31 ifikapo mwaka 2016 iwapo shughuli za kurutubisha madini ya uranium katika eneo la Yongbyon zitaendelea.

Hata hivyo, bado haijafahamika wazi ni lini shughuli za kurutubisha madini ya uranium, zitaanza. Waangalizi wengi wanaamini kuwa Korea Kaskazini imekuwa inarutubisha madini ya uranium kwa siri katika kiwanda chake kwa miaka kadhaa na kwamba jaribio la kombora la nyuklia lililofanywa na nchi hiyo mwezi Februari mwaka huu, huenda lilikuwa ni bomu la nyuklia. Jaribio hilo lilifanyika ikiwa ni katika kujibu mashambulizi baada ya Umoja wa Mataifa kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vipya.

Aina ya ndege za kivita za F22
Aina ya ndege za kivita za F22Picha: Getty Images

Jana Jumatatu, Rais mpya wa Korea Kusini, Park Guen-Hye, aliahidi kujibu mashambulizi iwapo Korea Kaskazini itafanya uchokozi wowote na kwamba mashambulizi hayo hayatazingatia madhara ya kisiasa. Jumamosi iliyopita, Korea Kaskazini ilitangaza kuwa inaingia katika hali ya vita na Korea Kusini na kuzionya Korea Kusini na Marekani kwamba uchokozi wowote ule utachochea moto na kuwa vita kamili vya nyuklia. Vitisho hivyo, vimepuuziwa na Marekani, ambapo jana imetangaza kupeleka ndege zake za kivita aina ya F-22 katika ngome ya kikosi cha anga ya Marekani huko Osan, ikiwa ni sehemu ya mazoezi ya kijeshi yanayoendelea kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE,RTRE
Mhariri: Josephat Charo