1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongozi wa upinzani Zimbabwe Morgan Tsangirai aondoa kesi ya kupinga uchaguzi

17 Agosti 2013

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsangirai ameondoa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Urais nchini humo uliofanyika mwezi uliopita uliompa ushindi Rais Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/19RKt
Picha: Alexander Joe/AFP/Getty Images

Msemaji wa chama cha Movement for Democratic change MDC Douglas Mwonzora amesema waziri mkuu huyo wa Zimbabwe ameamua kuondoa kesi hiyo mahakamani kwasababu anahisi haitatendewa haki kutokana na vizingiti vilivyoko kisheria.

Tsangirai amesema hakuwa na budi bali kuondoa kesi hiyo iliyokuwa imepangwa kusikizwa leo(17.08.2013) baada ya tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kukosa kumpa nakala alizohitaji katika kuwasilisha hoja zake mahakamani za kupinga uchaguzi huo.

Mugabe kuapishwa bila pingamizi

Kuondolewa kwa kesi hiyo sasa kunatoa fursa ya kuapishwa kwa Rais Mugabe mwenye umri wa miaka 89 kwa awamu ya saba madarakani bila pingamizi.Mugabe ameliongoza taifa la Zimbabwe kwa miaka 33 tangu mwaka 1980 nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru kutoka Uingereza.

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe
Rais wa Zimbabwe Robert MugabePicha: Reuters

Mugabe na Tsangirai wamekuwa katika serikali ya mseto tangu mwaka 2008 baada ya uchaguzi uliozua utata na kulazimu kuundwa kwa serikali ya kugawana madaraka.

Tsangirai amepinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe 31 mwezi Julai ambao tume ya uchaguzi ilitangaza alipata asilimia 34 ya kura zilizopigwa, huku Mugabe akishinda kwa asilimia 61 ya kura.Tsangirai amedai uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu na alitaka ufanyike upya.

Mahakama ya kikatiba ilikuwa inapangiwa kusikiza hoja za chama cha MDC leo ili kuamua iwapo kesi hiyo iendelea mbele.Wakili wa Mugabe Fred Gijima hata hivyo amesema kesi hiyo itaendelea licha ya kuondolewa na Tsangirai na kuongeza kuwa chama cha MDC hakiwezi tu kujiondoa kutoka kesi hiyo baada ya kutoa madai yenye uzito ya kuibiwa kwa kura.

Mataifa ya magharibi yashutumiwa

Wakati huo huo,Mugabe kwa mara nyingine ameyashutumu mataifa ya magahribi alipowasili katika mkutano wa viongozi wa kanda hiyo ya kusini mwa Afrika nchini Malawi.

Mugabe amewaambia wanahabari kuwa nchi za magharibi zinataka kuwaza kwa niaba yao, kuchukua maamuzi na hata kuziambia nchi za Afrika mkondo gani wa kuchukua.

Bango lililo na ujumbe wa madai ya kuibiwa kwa kura Zimbabwe
Bango lililo na ujumbe wa madai ya kuibiwa kwa kura ZimbabwePicha: AP

Kulingana na Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma, jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika SADC yenye nchi wanachama 15 itachapisha ripoti yake kuhusu uchaguzi wa Zimbabwe katika mkutano huo wa mwishoni mwa juma hili.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka kanda hiyo wamesema uchaguzi huo ulikuwa huru lakini hawajazungumzia iwapo ulikuwa wa haki.Zuma amesema walichokuwa wakitaka ni uchaguzi wa amani na huru na kusema hilo lilifikiwa.Alikuwa akizungumza mjini Lilongwe nchini Malawi.

Lakini chama cha MDC kimewasilisha malalamiko yao kwa SADC ambayo ilipatanisha pande hizo mbili na kusababisha ugavi wa madaraka mwaka 2008.Naibu kiongozi wa chama hicho Thokozani Khupe na afisa wa ngazi ya juu wa chama hicho Jameson Timba pia wamesafiri kwenda Malawi kuwasilisha kesi yao ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwa viongozi hao wa SADC.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Sekione Kitojo