1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongo yailaumu Uganda kwa kuvunjika mazungumzo

12 Novemba 2013

Ujumbe wa serikali ya Kongo umejiondoa katika mazungumzo na waasi wa M23 yanayosimamiwa na Uganda, baada ya pande hizo mbili kutofautiana kuhusu vipengele vya muafaka wa amani uliolenga kumaliza uasi Kongo

https://p.dw.com/p/1AFkj
Naibu waaziri wa mambo ya nchi za nje wa Uganda Okello Oryem akizungumza na waandishi habari wa shirika la AP baada ya kushindwa kutiwa saini makubaliano ya amani ya KongoPicha: Getty Images/Afp/Phil Moore

Msemaji wa serikali Lambert Mende amesema "Uganda inaonekana kuchangia kama sehemu ya mgogoro huo. Inaegemea upande wa M23".

Kwa mujibu wa naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Uganda, Okello Oryem, makubaliano hayo yanatarajiwa kutiwa saini. Hata hivyo hajazungumzia madai kuwa Uganda inawaunga mkono waasi.

"Pande zote mbili bado ziko nchini Uganda....Mazungumzo hayajavunjika",msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amesema hayo mbele ya waandishi wa habari mjini Kampala.

Kushindwa dakika ya mwisho kutiwa saini makubaliano ya amani,lilikuwa pigo kwa juhudi za kimataifa za kumaliza mzozo katika eneo la mashariki la jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali,waziri wa ulinzi wa Uganda Crispus Kiyonga aliendelea na juhudi za upatanishi usiku kucha pamoja na pande zote mbili husika.

Kongo Militäraktion gegen M 23 Rebellen
Wanajeshi wa Kongo wamewekwa karibu na Bunagana baada ya M23 kutimuliwaPicha: Reuters/Kenny Katombe

Serikali ya Kinshasa inataka kudurusu makubaliano

Mazungumzo yalikwama baada ya serikali ya mjini Kinshasa kudai marekebisho katika waraka wa makubaliano.Hata hivyo licha ya kutotiwa saini,waziri wa mambo ya nchi za nje wa jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Raymon Tshibanda amesisitiza serikali imedhamiria kufikia amani.

Uganda ambayo ndiyo mwenyeji na mpatanishi wa mazungumzo hayo ya muda mrefu imesema inataraji mazungumzo yataendelea,lakini haikusema lini.

"Ujumbe wa DRC utakapokuwa tayari,wapatanishi watakuarifuni tarehe mpya",msemaji wa serikali ya Uganda Ofwono Opondo amesema.

M23 wamesema katika taarifa yao kwamba serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo imetaka kudurusu waraka uliokuwa umeshakubaliwa na pande zote mbili-na kusema madai hayo ya serikali hayakubaliki kwakua makubaliano yalikuwa yameshapangwa tangu mapema mwezi huu na vigezo vya kabla ya kutia saini vimeshakamilishwa".

Hata hivyo tangu wakati huo,waasi wa M23 wameshindwa vibaya sana katika uwanja wa mapigano na pigo hilo limebadilisha hali ya mambo na kuwaacha wanajeshi wa serikali wakidhibiti hali ya mambo.

Martin Kobler bei einer Pressekonferenz im Kongo
Mjumbe maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Martin Kobler akizungumza na waandishi habariPicha: Junior D.KannahAFP/Getty Images)

Matumaini ya amani hayajatoweka

Watu wengi wamevunjika moyo kutokana na makubaliano ya amani kutotiwa saini jana-walitaraji ingekuwa hatua muhimu kuelekea amani katika eneo hilo la mizozo.

Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa katika eneo la maziwa makuu Mary Robinson na mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa katika jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Martin Kobler wameelezea masikitiko yao kwa kushindwa kutiwa saini makubaliano ya amani.Hata hivyo wamesema pande zinazohusika "hazikutaja tofauti zozote kuhusu mada zilizomo katika waraka wa makubalino.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na bibi Mary Robinson na Martin Kobler na kutiwa saini pia na maafisa wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, inazihimiza pande husika zisawazishe tofauti zilizoko na kuwajibika katika juhudi za kuupatia ufumbuzi wa amani mzozo. "Wote wamesisitiza ufumbuzi wowote unabidi uruhusu wahalifu wa vita waandamwe kisheria.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP

Mhariri: Josephat Charo