Kongamano la vyombo vya habari lamalizika Bonn
21 Juni 2017Wachangiaji kutoka kote ulimwenguni walikusanyika kandoni mwa Mto Rhine hapa Bonn, kujadili mustakabali wa vyombo vya habari katika zama zetu, kuanzia wenye majina makubwa kama Jeff Mason, rais wa waandishi wa Ikulu ya Marekani, waliotunukiwa tuzo ya mwaka huu ya uhuru wa habari, hadi wasanii kutoka Afrika, wamiliki wa vyombo vya habari kutoka Asia na wavumbizi na wanafalsafa kutoka Marekani ya Kusini na Ulaya.
Akizungumza na washiriki waliokusanyika kwenye ukumbi wa jengo la zamani la bunge la Ujerumani Magharibi, Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, alisema uandishi wa habari wa sasa unakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa hapo zamani.
"Leo tunajikuta kwenye nyakati za mashaka sana, ambazo zinazigusa kazi zetu moja kwa moja. Utangazaji wa kimataifa unashuhudia mageuzi makubwa. Kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ukandamizaji kwenye mataifa moja moja na utangazaji wa kimataifa."
Kongamano la mwaka huu limeendeshwa chini ya maudhui kuu ya "utambulisho na mchanganyiko wa kijamii", lengo likiwa kuutambua na kuupa nafasi yake utambulisho wa kila tamaduni duniani, lakini wakati huo huo wenye tamaduni hizo wakikumbushwa kufurahikia na kuuheshimu mchanganyiko wa kiimani, kiitikadi na kimfumo ambao ndio hasa unaouumba ulimwengu.
"Nimejifunza kwamba jamii ni mkusanyiko wa tamaduni nyingi na imani mbalimbali, kwa hivyo sisi kwenye vyombo vya habari tunapaswa kuwasaidia wanajamii kutambua ukweli huo na kuishi pamoja kwa amani," anasema Passy Mubalama, mwandishi wa blogu kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akisisitiza kuwa kuwa kongamano hili limempa funzo kubwa la utangamano wa kijamii.
Miongoni mwa mada ambayo ilichukuwa sehemu kubwa ya mjadala ni ile inayohusiana na "taarifa za uzushi" kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo limeathiri siasa za kitaifa na kimataifa ulimwenguni.
Brian Obara Wangoma, mmoja wa waendeshaji wa mtandao wa This Is Africa akitokea nchini Kenya, mtandao ambao una lengo la kuonesha sura chanya ya bara la Afrika, ikilinganishwa na taswira mbaya iliyozoeleka katika kulielezea bara hilo tajiri kabisa kwa rasilimali duniani, anasema kuwa kuzitenganisha taarifa za uzushi na zile za ukweli ndilo changamoto kubwa nchini kwake, wakati huu taifa hilo la Afrika Mashariki likielekea kwenye uchaguzi.
Siku tatu za washiriki 2000 kutoka mataifa 130 kote ulimwenguni kukutana kwenye majengo ya ukumbi wa kimataifa wa mikutano, WCCB, na Deutsche Welle, hapa Bonn, ndiyo zimemalizika hivi kwa mwaka huu, ikiwa ni mara ya kwanza kwa washiriki kujadili mada zaidi ya 80, kuanzia "usalama wa kidijitali na ulinzi kwa waandishi wa habari na wachambuzi" hadi "ukuwaji wa siasa kali za mrengo wa kulia duniani" kwa wakati mmoja.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman