Kongamano la serikali kuhusu kilimo nchini Kenya
19 Januari 2022Waziri wa kilimo,mifugo na uvuvi na vyama vya ushirika nchini Kenya Peter Munya amethibitisha kuwa kipo chakula cha kutosha nchini ambacho kwa sasa kinaendelea kusambazwa katika maeneo mbalimbali ya Kenya kuwasaidia wanaokabiliwa na baa la njaa.
Ukame unaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini Kenya,hasa katika eneo la kaskazini mashariki. Ukame umesababishwa na kuchelewa kwa mvua na pia kukosekana kwa mvua ya kutosha hali iliyochangia maelfu ya raia kukosa chakula na maji,
''Hatuna shida ya chakula''
DW Kiswahili imepata fursa ya kuzungumza na Waziri wa Kilimo, mifugo na uvuvi wa Kenya Peter Munya ambaye ameelezea juu ya mikakati inayoendelea kuwasaidia wakenya wanaokabiliwa na njaa. Waziri Munya amesema hakuna uhaba wa chakula cha msaada na kwamba wote walioathirika na ukame watapata chakula na maji.
"Chakula inatosha ile tumelima na ile nyengine inatoka nje ya Kenya iko,hata wakulima hawajauza bado,kuna wakulima wameshikilia chakula,kwa hivyo hatuna shida ya chakula",alisema Munya.
Waziri Munya aidha amedokeza kwamba serikali bado inatoa pesa kwa wale ambao wana shida ya chakula na pia idara ya miradi maalumu inaendelea kugawa chakula kwa Wakenya wote walioathirika na hawana mahali pa kununua. Vile vile waziri Munya amesema kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa mifugo pia wanapata chakula ili kuepusha vifo vya mifugo wakati wa kiangazi,
"Tumepeana idhini kwa wale ambao wanatengeneza chakula ya ngombe wanunue mahindi inayoitwa yellow maize watengeneze chakula cha ngombe na wako kwa process ya kutengeneza chakula cha ngombe.", aliendelea kusema Munya.
Kiangazi na mifugo wakosa malisho
Kwa upande wake gavana wa Kiambuu ambaye pia ni mwanauchumi wa kilimo nchini Kenya James Nyoro amesema kuwa kama baraza la magavana nchini Kenya wameshirikiana na wizara kuweka mikakati kuhakikisha nchi ina usalama wa upatikanaji wa chakula na Wakenya wanaoishi katika maeneo yenye ukame wanapata chakula badala ya kutegemea misaada.
Maelfu ya wakenya wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa chakula wakati wa kiangazi na mifugo kufa kutokana na kukosa malisho na maji,lakini wizara ya kilimo,mifugo na uvuvi nchini Kenya inasema inajaribu kila mbinu kuhakikisha kuwa suluhu ya kudumu inapatikana.