1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kuokoa bahari lafunguliwa rasmi mjini Lisbon

Thelma Mwadzaya27 Juni 2022

Kongamano la masuala ya bahari limefunguliwa rasmi mjini Lisbon nchini Ureno. Kenya na Ureno ndio wenyeji wa Kikao hicho cha mazingira.

https://p.dw.com/p/4DJgT
2022 UN-Ozeankonferenz
Picha: Carlos Costa/AFP

Kauli Mbiu inajikita kwenye juhudi za kuimarisha harakati za kuinusuru bahari kupitia sayansi na teknolojia. Wakenya waishio pwani wana mchango muhimu katika harakati hizo.

Kongamano hilo la masuala  ya bahari linafanyika wakati ambapo jamii inajijenga upya baada ya janga la COVID 19 kuuzindua ulimwengu mintarafu mabadiliko ya tabia ya nchi.

Bahari ina uwezo mkubwa wa kufyonza hewa kaa ambayo inasadikika kuchangia katika ongezeko la viwango vya joto duniani. Katika eneo la Kuruwitu la kaunti ya Kilifi, wahifadhi wa mazingira ya bahari walianzisha mradi wa Kutengeza matumbawe ya Saruji ili kuyanusuru maeneo ambayo ni mazalio ya samaki.

2022 UN-Ozeankonferenz
Rais Uhuru Kenyatta akiwa na viongozi wengine katika mkutano wa bahariPicha: Carlos Costa/AFP

Charo Hinzano ni mwanamazingira na mlinzi wa bahari kutokea pwani. Yeye Anahusika kwa karibu na mradi wa kutengeza matumbawe wa shirika la Oceans Alive na amesema Matumbawe ni muhimu kwenye uhai wa bahari ukizingatia kuwa ni makaazi ya viumbe mbalimbali.

Kikao cha Lisbon kina ratiba inayojikita kwenye sehemu 4 ambazo ni vijana, Uchumi endelevu wa bahari, muingiliano wa bahari na mito au maziwa yaliyo na maji ya baridi Pamoja na harakati za kijamii katika nyanja zote.

Mkutano huo utawawezesha wadau kuwa na kauli moja ya kuunda mbinu endelevu za biashara ya rasilmali za bahari kadhalika kuleta uwiano kati ya sera, mipango na sekta ya binafsi. Mwanaharusi Mwafrika ni mratibu wa mradi wa kuhifadhi mikoko kutokea eneo la Vanga na anaelezea mchango wa vijana katika harakati za uhifadhi wa mazingira ya baharini. 

Uvuvi ni shughuli muhimu kwa wakaazi wa ukanda wa pwani na kitega uchumi. Ijapokuwa hatua zimepigwa kuwaelimisha wavuvi kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira kazi Bado ipo. Mkutano huo wa Lisbon unakamilika Julai Mosi. Kenya inapania kuwa na sauti kubwa zaidi kwenye masuala ya Uchumi wa bahari.