Kongamano la Kimataifa la Wanahabari Bonn
13 Juni 2016Siku hii ya ufunguzi imeambatana na utowaji wa tuzo ya uhuru wa kujieleza ya Deutsche Welle, ambayo mwaka huu ametunukiwa mhariri wa gazeti la Hurriyet la Uturuki, Sedat Ergin, na ambaye kwa sasa anakabiliwa na kesi mahakamani kwa kosa la kumkashifu Rais Tayyip Erdogan.
Akizungumza kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Bonn, kunakofanyika kongamano hili, Mkurugenzi Mkuu wa Deutsche Welle, Peter Limbourg, amesema tuzo kwa Ergin ni alama ya kuungana na waandishi wote duniani wanaokabiliwa na tawala zisizo tayari kusikia maoni huru.
"Nadhani hii si nishani tu kwa Sedat Ergin, bali pia ni kwa ajili ya kila mwandishi wa habari nchini Uturuki na kwengineko, ambao wanaishi chini ya vitisho vya serikali, vitisho vya polisi wa siri, na hata vitisho vya majaji ambao huwasaidia watawala kukandamiza uhuru wa habari kwenye nchi zao," alisema Limbourg.
Gauck ahimiza maadili
Mapema akiwakaribisha wageni wa kimataifa kwenye kongamano hili la siku tatu, Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck, alisema "kama yalivyo, maudhui ya kongamano hili la mwaka huu: Vyombo vya Habari. Uhuru. Maadili." yanataka watu wajadiliane kwa kina, hata kama hawakubaliani, hasa juu ya ukweli kuwa ulimwengu unaishi kwenye zama za mawasiliano ya mitandao, ambayo kuwa kwake huru ni muhimu sawa ilivyo na kuwa kwake ya kimaadili.
"Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la taarifa zinazopatikana mitandaoni, sisi kama wanaadamu tunapaswa kuwa na mdahalo juu ya maadili na matayarisho yanayoelezea namna zetu za kufikiri, kuzungumza na namna pia tunavyoalakiana baina yetu."
Kongamano hili linawakutanisha pamoja washiriki zaidi ya 2,000 kutoka pande zote za dunia, yakiwamo mataifa ya Afrika Mashariki. "Nimekuja kujifunza na ninaamini nitaondoka na mengi juu ya nafasi ya vyombo vya habari kwenye demokrasia na haki za binaadamu," anasema Eva Solomon, msaidizi wa mkuu wa Chuo cha Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania.
Pamoja na ufunguzi, siku ya leo pia ilitandwa na mijadala 12 kwenye vipindi na vikao mbalimbali, ukiwemo mjadala juu ya nafasi ya mitandao ya kijamii katika kuinua uhuru na haki za kibinaadamu katika mataifa ya dunia ya tatu.
Kongamano hili la Kimataifa la Vyombo vya Habari linaendelea tena hapo kesho na kumalizika keshokutwa.
Mwandishi: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga