1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Fasihi

Wataalamu wajadili Kiswahili Zanzibar

Salma Said21 Desemba 2017

Kongamano la Kiswahili la kimataifa limefayika Zanzibar na kuwakutanisha wataalamu waliobobea kwenye lugha hiyo kutoka nchi mbali mbali zikiwemo za Afrika Mashariki, Marekani, Ujerumanibna Misri.

https://p.dw.com/p/2pmVp
Dr. Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar, Dk,Ali Mohammed Shein akizindua kongamano la kwanza la kimataifa la Kiswahili katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani Kikwajuni Zanzibar, 21.12.2017. Picha: DW/S.Said

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein amesema wakati akifungua kongamano hilo, kwamba lengo la mkusanyiko huo ni kuyaendeleza matukio muhimu mawili ya kihistoria katika jitihada za kuikuza na kuiendeleza lugha adhimu ya Kiswahili ambapo mambo mawili muhimu yanayopaswa kuzingatiwa katika kongamano hilo ni historia, ambayo inatambuliwa kwamba Zanzibar ndio chimbuko la Kiswahili.

Mnamo mwaka 1930, Wakoloni waliamua kukichukua Kiswahili cha Unguja Mjini na kukifanya kuwa ndicho Kiswahili rasmi na sanifu, ili kitumike katika ukanda wote wa Afrika ya Mashariki.

Jambo la pili ni kuwa mwaka huu wa 2017, Jumuiya ya Afrika Mashariki iliichagua Zanzibar kuwa makao ya Ofisi ya Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki na kwa muktadha huo mambo yote hayo yanaiongezea heshima Zanzibar katika jitihada za kuiendeleza lugha ya Kiswahili duniani.

Dk Shein alisema Kiswahili ni lugha yenye ladha inayopendeza na kukisisimua kinywa cha msemaji na thamani yake ni kubwa sana miongoni mwa lugha nyingi hapa duniani. Katika ukuaji wa lugha ya Kiswahili ni vigumu kuusahau mchango mkubwa wa utamaduni na mila za waswahili.

Ukuaji wa kiswahili umekuwa ukiendelezwa katika nchi tofauti duniani ambapo sasa nchi nyingi zimeshaunda vyama vyao vya Kiswahili.

Sansibar - Dr. Ali Mohammed Shein eröffnet das erste Internationale Kishwahili Symposium
Rais wa Zanzibara Dk. Ali Mohammed shein akikunjuwa Kitambaa kinachoonesha picha ya mtunzi mahiri wa vitabu na alieneza lugha ya Kiswahili, Muhammed Said Abdulla, alipowasili ndani ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi la zamani kwa ajili ya uzinduzi wa kongamano la kwanza la kimataifa la Kiswahili Kikwajuni, Zanzibar, 21.12.2017.Picha: DW/S. Said

Akitoa salamu za vyama vya Kiswahili Duniani, (CHAUKIDU) Dk Mahir Mwita ametoa wito kwa waendelezaji wa Kiswahili kuiendeleza lugha hiyo ili kuwavutia wale wasiotumia lugha ya kiswahili waweze kujifunza zaidi na hilo ni miongoni mwa kazi za vyama vyao.

Licha ya kuendelezwa na kusomeshwa katika vyuo mbali mbali duniani lugha ya Kiswahili Profesa Alywiya Saleh Omar anasema kunahitajika mbinu mpya za kusomeshea.

Mohammed Seif Khatib, Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) amesema waandishi wa riwaya na vitabu wa Zanzibar wamefanya kazi kubwa katika kuitunza na kuitumia lugha adhimu ya Kiswahili na kuijengea heshima kubwa ndani na duniani kwa ujumla.

Katika kongamano hilo kumefanyika Mjadala maalumu uliopewa jina la wazungu njooni wenyeji wapone hali na mustakabali wa programu za Kiswahili kwa wageni ughaibuni na Afrika Mashariki ambao umewashirikisha wabobezi wa Kiswahili kama Dkt Mahir Mwita , Bibi Zainab Ali Iddi, Professa Kiarie Wanjogu, na Dkt Leonard Muaka

Mwandishi: Salma Said

Mhariri: Saumu Yusuf