Komorowski ashinda uchaguzi wa rais Poland
5 Julai 2010Kwa mujibu wa televisheni ya taifa TVP, Komorowski amejikingia asilimia 53 ya kura zilizopigwa wakati mpinzani wake, Jaroslaw Kaczynski amepata asilimia 47.
Kaczynski ni kiongozi wa chama kikuu cha upinzani kinachofuata sera za mrengo wa kulia, "Law and Justice" na ni ndugu pacha wa rais Lech Kaczynski alieuawa katika ajali ya ndege mwezi wa Aprili.Uchaguzi wa rais umeitishwa kufuatia kifo hicho.
Matokeo ya uchaguzi huo humaanisha kuwa Komorowski wa chama cha kiliberali cha "Civic Platform" na mshirika wake wa karibu, Waziri Mkuu Donald Tusk wataweza kuidhinisha marekebisho ya kifedha kabla ya uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanywa mwakani.
Kwa mujibu wa Katiba ya Poland, wajibu wa rais sio kuliwakilisha taifa tu bali ana mamlaka yake hasa katika sera za nje na usalama. Jaroslaw Kaczynski amekubali kuwa ameshindwa na amempongeza mpinzani wake Komorowski.
Mwandishi:P.Martin/RTRE/DPA
Mhariri: Mwadzaya,Thelma