1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombora la Korea Kaskazini lapita anga ya Japan

29 Agosti 2017

Shirika la Utangazi la Japan, NHK limesema kuwa Korea Kaskazini imerusha kombora ambalo limepita katika anga ya Japan, hali iliyosababisha tahadhari kutolewa kwa watu wa eneo hilo.

https://p.dw.com/p/2j0En
Nordkorea Raketenstart
Picha: picture-alliance/dpa/Kcna

Shirika la Utangazi la Japan, NHK limesema kuwa Korea Kaskazini imerusha kombora kupita anga ya Japan, hali iliyosababisha tahadhari kutolewa kwa watu wa eneo hilo. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa utakutana kwa dharura leo mchana kujadili suala hilo.

Kwa mujibu wa shirika Utangazi la Japan, kombora hilo lililopita nchini humo mapema leo asubuhi, lilivunjika vipande vitatu na kuangukia baharini katika kisiwa cha Hokkaido kilichoko kaskazini mwa Japan.

Jeshi la Korea Kusini limesema kuwa kombora hilo lilirushwa kutoka kwenye mkoa wa Sunan, karibu na mji mkuu wa Korea Kaskazini, Pyongyang na liliruka umbali wa kilomita 2,700.

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe amelaani kitendo hicho akisema ni cha uchokozi usio wa kawaida na kwamba ni kitisho kikubwa chenye madhara kwa amani na usalama wa ukanda huo. Waziri wa baraza la mawaziri na msemaji mkuu wa serikali nchini Japan, Yoshide Suga amekielezea kitendo hicho kuwa ni ukiukwaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.

Abe amesema Japan imeomba kufanyika kwa mkutano wa dharura na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa baadae leo mchana mjini New York kwa ajili ya kuimarisha hatua za kuchukua dhidi ya Korea Kaskazini.

USA Besuch Shinzo Abe in Washington
Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo AbePicha: picture-alliance/dpa/A. Harnik

Abe ambaye amezungumza na Rais wa Marekani, Donald Trump kwa njia ya simu amesema wamekubaliana kuweka shinikizo zaidi kwa Korea Kaskazini. Amesema Trump amemuhakikishia kuwa nchi yake inasimama na Japan kwa asilimia 100.

''Japan na Marekani zimekuwa na msimamo wa pamoja katika suala hili. Hatua ya Korea Kaskazini kurusha kombora inaleta kitisho kikubwa na haikubaliki. Hivyo tumekubaliana kuomba kikao cha dharura katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haraka iwezekanavyo ili kuongeza shinikizo dhidi ya Korea Kaskazini, alisisitiza Abe.''

Wakurugenzi wa usalama wazungumza

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Japan na Marekani pamoja na wakurugenzi wa usalama pia walikuwa na mazungumzo ya simu kutokana na hatua hiyo iliyofanywa na Korea Kaskazini.

Serikali ya Japan imewaonya wananchi wake walioko kaskazini mwa nchi hiyo kupitia mfumo wa tahadhari, redio na vipindi vya televisheni na imewashauri wachukue tahadhari. Jeshi la taifa la kisiwa hicho kwa sasa linafanya majaribio ya kupeleka mitambo ya kuzuia makombora katika kambi tatu za jeshi la Marekani zilizoko nchini Japan.

Katika hatua isiyo ya kawaida, Korea Kusini pia imechapisha picha za majaribio ya makombora yake ya masafa marefu na imesema yalirushwa wiki iliyopita. Jeshi la nchi hiyo limetoa taarifa inayoionya Korea Kaskazini kujizuia kufanya mashambulizi zaidi ya uchokozi. Picha hizo zinaonyesha aina mbili ya makombora mapya yanayoweza kuruka umbali wa kilomita 800 na 500.

Japan Raketenabwehrsystem PAC 3 in Fussa
Mitambo ya kuzuia makombora ya JapanPicha: Reuters/I. Kato

Urushwaji wa kombora hilo umetokea siku chache baada ya Korea Kaskazini kurusha makombora matatu ya masafa mafupi mwishoni mwa juma, hatua ambayo ilikosolewa vikali kimataifa. Hata hivyo, Korea Kaskazini kurusha makombora kupitia anga ya Japan ni kitendo kisicho cha kawaida.

Kwa upande mwingine, Urusi imesema ina wasiwasi sana kuhusu jinsi Korea Kaskazini inavyozidi kutanua maeneo inayorusha makombora yake. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Ryabkov amesema kuwa wameiona tabia hiyo ya Korea Kaskazini na ina wasiwasi kuhusu maendeleo hayo kwa ujumla.

Wakati huo huo, mke wa kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jon Un, amejifunga mtoto wao wa tatu. Imeripotiwa kuwa idara ya intelijensia ya Korea Kusini jana iliiarifu kamati ya intelijensia ya bunge la nchi hiyo kwamba mtoto huyo alizaliwa mwezi Februari, ingawa jina na jinsia yake bado havijajulikana.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga