1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la super cup la Afrika kuchezwa Addis Ababa

Ramadhan Ali8 Septemba 2006

Kombe la Super cup mwakani litaaniwa addis Ababa, ethiopia kuadhimisha mwaka wa 50 wa kuasisiwa kwa shirikisho la dimba la Afrika na Misri,Ethiopia,sudan na Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/CHdD

Baada ya changamoto za kati ya wiki za kuania tiketi za finali ya Kombe lijalo la Ulaya la kimataifa ambamo Ujerumani iliizaba San Marino mabao 13 :0, jumamosi hii ni duru ya kwanza ya kuania kombe la Taifa la Ujerumani-DFB Pokale:Mabingwa ni bayern Munich ambao pia ni mabingwa wa kombe la Ligi.Wanaingia uwanjani leo bila ya nahodha wao –kipa Oliver kahn na mahasimu wao leo ni wale wale waliowatoa jasho msimu uliopita- St.Pauli.

Klabu hiyo ya hamburg ndio ililazwa na munich mabao 3:0 katika nusu-finali, lakini Munich ilitia mabao yake 2 kati ya 3 mnamo dakika 6 za mwisho.,Alikua Claudio Pizarro wa Peru alieokoa jahazi.Basi katika uwanja wa Reeperbahn leo,Munich imepata salamu za msimu uliopita.

Oliver kahn hachezi leo kwa kuwa amefungiwa mechi moja wakati wa finali ya kombe hili mwaka jana kati ya Munich na Frankfurt.Munich ilishinda kwa bao 1:0.

Katika mapambano mengine ya leo, Energie cottbus ya mashariki mwa ujerumani iliopanda daraja ya kwanza msimu huu ina miadi na Rot-Weiss Essen wakati bayer Leverkusen wanakutana na Koblenz.Hannover inacheza na Dynamo Dresden.Hannover ndio inayoburura sasa mkia wa Ligi ya kwanza ya Bundesliga.Kesho kinyan’ganyiro hiki kinaendelea.FC Cologne ilioteremshwa daraja ya pili inacheza na Carl Zeis Jena,Ahlen na Duisburg wakati Fc Bremerhaven inachuana na Wolfsburg.

Kocha wa Ufaransa Raymond Domenech anaweza sasa kusahau pigo iliopta Ufaransa kutoka kwa Itali katika finali ya Kombe la dunia.Ufaransa kati ya wiki hii iliilaza Itali kwa mabao 3:1 mjini Paris,ikicheza na Claude makelele,shina la mvutano kati ya domenech na kocha wa Chelsea-Jose Mourinho.

“makelele anasema atakayo kusema, Chelsea nayo inasema itakayokusema na mimi nafanya ninavyotaka kufanya.” Alinukuliwa Raymond Domenech kusema.Mvutano huu umechomoza kwavile kocha Domenech anamshikilia Claude Makelele kuendelea kuichezea Ufaransa wakati binafsi angependa kustaafu kufuatia Kombe lililopita la dunia na kuendelea kuichezea klabu yake ya uingereza ya Chelsea.

Chini ya sheria za FIFA, Makelele aweza kufungiwa kuichezea Chelsea ikiwa atakataa kuichzea Ufaransa,endapo akichaguliwa.

Finali ya mwakani ya Super Cup-kombe la mabingwa wa Afrika, itakua mjini Addis Ababa,Ethiopia ikiwa sehemu ya maadhjimisho ya mwaka wa 10 tangu kuasisiwa kwa CAF-shirikisho la dimba la Afrika.CAF imetangaza kwamba, mechi hiyo itachezwa hapo februari,lakini haikutaja tarehe hasa.Hii itakua ni mara ya 4 kwa changamoto hii inayowa kutanisha kila mwaka washindi wa Kombe la klabu bingwa na wa kombe la shirikisho, kuchezwa katika uwanja usiozihusu timu zote mbili.

Sherehe za kuadhimisha nusu karne ya CAF zitajumuisha pia mpambano wa kirafiki mabingwa wa Afrika Misri na Sweden, mjini Cairo,Februari,7,2007.Mashindano ya chipukizi chini ya umri wa miaka 23 yanapangwa pia kufanyika nchini Sudan,yakiingiza mataifa 4 yalioasisi shirikisho hili:Misri,Ethiopia,Sudan na afrika Kusini.

Kuna matumaini ya mzozo uliozuka kati ya Harambee Stars-timu ya taifa ya Kenya –na kocha wao mpya wa Taifa-kipa wa zamani wa Ufaransa,Bernard Lama,kupatiwa ufumbuzi. Kocha huyo baadae aweza kurudi Kenya kuiongoza harambee Stars katika changamoto ijayo ya kuania tikiti ya finali ya kombe la Afrika la mataifa 2008,nchini Ghana.

Kenya ina miadi na Angola.Lama alifunga virago vyake ghafula na kurejea Ufaransa kati ya wiki hii baada ya kulituhumu shirikisho la dimba la Kenya,KFF kushindwa kumpa mkataba na halafu akaweka masharti ya kutimizwa kabla hakurudi septemba 18.

Chanzo cha mzozo huu ni hiki:Katibu mkuu wa KFF Dan omino amearifu kuwa, KFF ilifikia mapatano nam kocha Lama mwezi uliopita kumlipa mshahara wake kila baada ya miezi 4,kumpatia maskani ya kukaa ,gari na simu.lama amesema lakini,bado hakupewa mkataba kutia saini na amebidi kufanya kazi kupindukia wakati bila ujira.Oktoba 7, Harambee Stars ,wanabidi kuingia uwanjani kwa mchuano wao na Angola, timu iliowakilisha Afrika katika Kombe la dunia hapa Ujerumani.

Tukituwama zaidi juu ya swali la makocha wa kigeni walioajiriwa na takriban timu zote za Afrika mashariki na kati-Ruanda,Tanzania,Kenya na hata Uganda, mwenyekiti wa zamani wa shirikisho la dimba la Tanzania na CAF-Abdullah Maamri,alikuwa Kampala hivi karibuni na muandishi wetu Omar Mutasa alizungumza nae iwapo makocha hawa wapya watafua dafu:

Katika ringi ya mabondia, bingwa wa dunia wa wezani wa juu Wladmir klitschko atatetea taji lake la IBF na muamerika Calvin Brock mjini New York hapo Novemba 11.

Brock, mwenye umri wa miaka 31, yuko ngazi ya tatu ya shirikisho la ndondi la IBF pamoja na WBA na hakushindwa katika mapambano 29.Klitschko-muukraine,mwenye kambi ujerumani, ameshinda mara 46 katika changamoto 50.

Nae mbabe wa zamani wa wezani wa juu,Evander Holyfield akijaribu kurejea ringini,ana miadi na mpuetorico Fres Oquendo hapo Novemba 10, siku moja kabla changamoto ya Klitschko na Calvin Brock.Changamoto hii itakua San Antonio,Texas.

Katika medani ya riadha, bingwa wa zamani wa mbgio za kasi za mita 100 na 200,muamerika Marion Jones,anatumai ataweza kushiriki sasa katika Kombe la dunia la riadha wiki ijayo na kwenye mashindano ya Shanghai,baadae mwezi huu.

Hii inafuatia kufutiwa mashtaka ya tuhuma za madhambi ya doping .Kombe la dunia la riadha litaaniwa Septemba 16-17 mjini Athens,Ugiriki wakati mashindano ya Shanghai yatakuwa Septemba 23.Mwishoni mwa wiki hii, wanariadha wa afrika mashariki –ethiopia na Kenya watakuwa uwanjani mjini Stuttgart,kusini mwa Ujerumani.

Kesho, bingwa wa mabingwa wa mbio za magari za fomula one- Michael Schumacher atazamiwa kutangaza kustaafu mwishoni mwa msimu huu.

Schumacher, ametawazwa bingwa mara 7 kuanzia 1994-2004.