1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kombe la Mataifa ya Afrika laanza rasmi Guinea ya Ikweta

18 Januari 2015

Gabon imechukua udhibiti wa kundi A baada ya duru ya kwanza ya ufunguzi jana Jumamosi(17.01.2015) katika mashindano ya 30 ya kombe la mataifa ya Afrika nchini Guinea ya Ikweta .

https://p.dw.com/p/1EMDx
Africa Cup Burkina Faso vs Gabun Aubameyang 17.01.2015
Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon akifurahia baoPicha: De Souza/AFP/Getty Images

Gabon iliishinda Burkina Faso kwa mabao 2-0, wakati wenyeji waliambulia kutoka sare bao 1-1 na Congo Brazzaville.

Gabon ilishinda mjini Bata, kwa magoli ya Pierre-Emerick Aubameyang na Malick Evouna.

Africa Cup Burkina Faso vs Gabun Kabore 17.01.2015
Burkina Faso wakipambana na GabonPicha: De Souza/AFP/Getty Images

Aubameyang , ambaye ni nahodha wa Gabon anayecheza soka nchini Ujerumani katika klabu ya Borussia Dortmund , alipachika bao hilo katika dakika ya 19 ya mchezo mjini Bata.

Hapo mapema wenyeji wa mashindano hayo Guinea ya Ikweta wakiwa na ndoto ya kuanza kampeni ya mashindano haya kwa ushindi , ndoto hiyo ilichafuliwa na goli la dakika za mwisho la Thievy Bifouma anayechezea katika timu ya Almeria nchini Uhispania dakika tatu kabla mpira kumalizika.

Ulikuwa mchezo wa nguvu uliochezwa mbele ya mashabiki 35,000 katika uwanja mjini Bata, katika mwanzo mzuri wa mashindano hayo ambayo yalihamishiwa nchini Guinea ya Ikweta dakika za mwisho kufuatia kujitoa kwa Morocco kutokana na hofu ya kusambaa kwa ugonjwa wa Ebola.

Kocha alalamika

Hata hivyo kocha wa Congo Claude Le Roy alikasirika baada ya timu yake kukwama katika barabara wakati wakielekea uwanjani kutokana na msongamano mrefu wa magari.

Fußball Afrika Cup Äquitorialguinea vs. Kongo
Mshambuliaji wa Guinea ya Ikweta Emilio NsuPicha: picture-alliance/dpa/Barry Aldworth/Backpage

"Tulikuwa tumekwama barabarani kwa muda wa dakika 65, katika joto la nyuzi joto 40 kwa hiyo iwapo mchezo wetu mwanzoni mwa mchezo ulikuwa hovyo, ni kwasababu ya hali hiyo, kocha huyo wa siku nyingi raia wa Ufaransa amesema.

"Kwa kawaida inachukua dakika 12. Shirikisho la kandanda barani Afrika CAF linapaswa kuzilinda timu zote katika mashindano haya na sio kutoziheshimu baadhi.

"Ni jambo jema kwamba Guinea ya Ikweta imeyaokoa mashindano haya , ni watu wazuri sana, lakini ni lazima tulinde haki."

Africa Cup Fans
Mashabiki katika michuano ya kombe la AfrikaPicha: I. Sanogo/AFP/Getty Images

Uwanja mjini Bata ulikuwa tayari umejaa rangi nyekundu wakati mashabiki kwa maelfu wa timu hiyo ya nyumbani wakifurahia sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo, ambayo yalihudhuriwa na rais Teodoro Obiang Nguema, rais wa nchi hiyo ndogo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.

Leo Jumapili (18.01.2015) mapambano yanaendelea katika kundi B ambapo mabingwa wa mwaka 2012 Zambia Chipolopolo wanakutana na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo na Tunisia baadaye itapimana nguvu na Cape Verde katika mji wa Ebebiyin.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Abdu Mtullya