Kombe la dunia:Matumaini ya Afrika yaelekezwa kwa Ghana na Ivory Coast
16 Juni 2010Tumewaona wenyeji Bafana Bafana walipomudu suluhu tu na Mexico ya bao 1:1, Algeria,ikatolewa kwa bao 1:0 na chipukizi Slovenia; simba wa nyika-Kameroun, walishindwa kunguruma katika mbuga za Kruger Park Afrika Kusini na ilichapwa bao 1:0 na mabingwa wa Asia Japan.Ni Black Stars, Ghana,bila ya stadi Michael Essien, waliokuwa wa kwanza kupepea bendera ya Afrika walipoitoa Serbia kwa bao 1:0.
Sasa timu gani ya Afrika, imetoa matumaini ya kufika duru ya pili ? na vipi matarajio ya kufika na kupindukia pale kameroun ikicheza na mzee Roger Milla ilipotamba 1990 huko Italia na Senegal ,ikicheza na nahodha Al haj Diouf, zilipowasili hadi robo-finali.
Hata Nigeria,haikufua dafu wala kuweka matumaini.Hili lakini sio ilisemekana ni Kombe la Afrika na kombe litabaki Afrika hapo Julai 11 ?
Afrika kusini, Bafana Bafana,walishangiria kutia bao la kwanza kabisa katika kombe hili la dunia walipocheza na Mexico.lilikuwa bao maridadi lililoashiria makubwa.Lakini, mashabiki wa Bafana bafana wakihanikiza kwa vuvuzela,mazumari yao,yalizimwa pale mnamo dakika ya 80 ya mchezo,Mexico ilipowatilia kitumbua chao mchanga na kusawazisha. Nafasi nyingi walizopata washambulizi wa afrika Kusini kuondoka na ushindi hawakuzitumia.
Simba wa nyika, wakirudi katika kombe lao la 6 la dunia,tangu kucheza mara ya kwanza Spain,1982,wamebainisha nao hata bila ya nahodha Samuel Eto-o aliyechukua usukani kutoka kwa nahodha wa zamani Rigobert Song,sio simba wa zamani.
Wameshinmdwa kunguruma na wamedhihirisha kwanini hawakufika mbali katika Kombe la Afrika,huko Angola.
Eto-o kama alivyolalamika mzee Roger Milla, bado hakuifanyia Kameroun lolote lenye maana kinyume na Barcelona na Inter Milan,timu alizotawazwa nazo mabingwa wa Spian,Itali na Ulaya.
Nigeria, ilikwisha pia bainisha katika Kombe la Afrika huko Angola, kwamba haina stadi kati ya uwanja mfano wa J.J Okocha au usoni kama Rashidi Yakin,wachezaji wenye fikra na ufundi wa kuchangamsha mchezo na kutia mabao.
Algeria, pengine, wanajuta kwanini waliwatoa mafirouni -Misri,mabingwa wa afrika, nje ya Kombe hili la dunia.Kwani, nani ajuwae,pengine Misri, ikipepea bora zaidi bendera ya Afrika.
Kushindwa mpambano mmoja hakuna maana ndio timu za Afrika zimeshatolewa duru ya kwanza:la,hasha.lakini sio dalili njema huonekana asubuhi ?
Dalili tulizoziona hadi sasa,hazitupi matumaini,kwamba Simba na Tembo wa Afrika watatamba barani mwao.
Kama katika Kombe lililopita la dunia,Black Stars-Ghana, ndio nyota pekee ilionawiri hadi sasa katika mawingu ya Afrika,kwani ndio ilioondoka hadi sasa na ushindi na pointi 3.
Ivory Coast,ingawa bila ya ushindi dhidi ya Ureno, haikuvunja moyo licha ya kuangukia tena kama 2006,katika kundi la kufa-kupona.
Kwa kutoka sare na Ureno 0:0, zote mbili zitategemea sasa ushindi wazi dhidi ya Korea ya kaskazini ili kuifuata Brazil kutoka kundi hili duru ya pili.
Ivory Coast,bila ya kuwa nahodha wao Drogba si fit sawa sawa, yatoa matumaini kwa Afrika. Ghana imeshapiga hatua moja kwenda duru ijayo kama ilivyofanya Kombe lililopita la dunia.
Ivory Coast na Ghana, simba wa nyika Kameroun, wakitusamehe, ndizo hadi sasa zilizotimiza matarajio kuwa ndio tumaini la Afrika 2010.
Mwandishi: Ramadhan Ali/AFPE
Uhariri: Othman Miraji