Kombe la dunia: Ufaransa na Ubelgiji zatinga nusu fainali
7 Julai 2018Ni mataifa matano tu ambayo yamewahi kushinda kombe la dunia zaidi ya mara moja. Hakuna hata moja litakuwa na nafasi ya kushinda taji hilo mwaka huu. Mabingwa mara tano Brazil na mabingwa mara mbili Uruguay waliondolewa katika kinyang'anyiro cha mwaka huu cha kombe la dunia jana Ijumaa katika robo fainali. Argentina, taifa jingine lililofanikiwa kutwaa taji hilo mara mbili , ilipokea kipigo katika duru ya mtoano ya timu 16 bora, wakati mabingwa mara nne Ujerumani waliayaaga mashindano haya katika awamu ya makundi.
Italia, ambayo pia ilishinda mara nne taji hili, hata haikuweza kufuzu kucheza katika fainali hizi, ikipoteza nafasi hiyo kwa Sweden katika michezo ya mchujo.
Hii ni mara ya kwanza kutakuwa na michuano ya nusu fainali bila ya takriban Argentina, Brazil, Ujerumani ama Italia.
Kwa sasa ni Ufaransa na England pekee kama mabingwa wa zamani ambazo bado zina nafasi ya kushinda taji hili nchini Urusi.
Brazil ilikuwa moja ya timu zilizopigiwa upatu wakati fainali hizi zikianza nchini Urusi, lakini Brazil ilisumbuka mapema katika awamu ya makundi kuonesha uwezo wake na hatimaye ilipoteza mchezo wake jana dhidi ya Ubelgiji kwa mabao 2-1 mjini Kazan.
Baada ya mwanzo wa kusua sua katika duru za kufuzu kucheza katika fainali hizi, Brazil ilimuondoa nahodha aliyeshinda kombe hilo la dunia mwaka 1994 Carlos Dunga na kumteua Tite kuwa kocha wa ikosi hicho. Tite alileta mabadiliko haraka katika matokeo ambayo yalisababisha Brazil ufuzu kucheza katika fainali hizi.
Licha ya kuwa Brazil ilimaliza ikiwa ya kwanza katika kundi E, ilishindwa kukonga nyoyo za mashabiki katika ushambuliaji. Kulikuwa na vitu vya hapa na pale kutoka kwa Neymar , ufundi na kasi pamoja na Philippe Coutinho, lakini timu haikuwa ikicheza kwa uhuru kuelekea golini kama wengi walivyotarajia.
Ngome ya Brazil
Kwa kiasi fulani ngome ya Brazil ilikuwa imara , ikiruhusu bao moja tu katika awamu ya makundi hadi katika awamu ya timu 16 bora. Brazil sasa imeondolewa na mpinzani kutoka bara la Ulaya katika awamu ya mtoano katika kila fainali nne za kombe la dunia tangu ilipoweza kutwaa kombe hilo mwaka 2002.
Uruguay ilikuwa mshindi wa kwanza wa kombe la dunia mwaka 1930 na nchi hiyo iliongeza taji la pili miaka 20 baadaye wakati ilipoishinda Brazil katika mchezo wa fainali mjini Rio de Janeiro.
licha ya kuwa Uruguay haijafikia katika fainali tangu wakati huo , wameweza kuwapo tena katika awamu za fainali.
Mwaka 2010 , Uruguay ilifika katika nusu fainali , na kupoteza dhidi ya Uholanzi kwa mabao 3-2. Timu hiyo ilifika karibu tena na awamu hiyo mwaka huu, lakini ilishindwa na Ufaransa jana kwa mabao 2-0 mjini Nizhny Novgorod.
Uruguay ilikuwa ya pili katika kundi la mataifa ya Amerika kusini kufuzu kucheza katika fainali hizi nyuma ya Brazil. Uwezo wake mkubwa iliyouonesha nchini Urusi mara hii, hususan katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ureno katika duru ya timu 16, ilipandisha matumaini kwamba timu hiyo inaweza takriban kufikia uwezo wake wa mwaka 2010.
Hata hivyo, wakati wa kipigo dhidi ya Ufaransa katika robo fainali, Uruguay ililazimika kucheza bila ya mshambuliaji wake aliyeumia Edinson Cavani. Na makosa makubwa aliyofanya mlinda mlango Fernando Muslera yalimzawadia Antoine Griezmann bao.
Leo michuano ya robo fainali ya mwisho inafanyika wakati Sweden inatiana kifuani na England na kisha wenyeji Urusi wataingia dimbani kuoneshana kazi na Croatia.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga