Kombe la dunia: Ni Ufaransa na Croatia katika fainali
15 Julai 2018Ufaransa pia itaongezwa nguvu kwa kujaribu kuweka kando hali ya kukatisha tamaa baada ya kushindwa katika fainali ya kombe la mataifa ya Ulaya Euro 2016 dhidi ya Ureno mjini Paris.
Ni fainali ambayo watu wachache walitarajia wakati tamasha hilo kubwa la kandanda duniani lilipoanza wiki nne zilizopita. Croatia imeleta furaha katika taifa hilo la Balkanambalo lina wakaazi milioni 4 tu kwa kuenda kinyume na hali ya kawaida na kusongambele hadi katika fainali wakati mabingwa watetezi Ujerumani , na kisha Argentina na Brazil ziliangukia pua nchini Urusi.
Wametiwa hamasa na mchezaji wa kati mtaalamu Luka Modric wakati kocha wake Zlatko Dalic , ambaye aliichukua timu hiyo mwaka jana tu wakati kikosi hicho kikiwa katika hali ya mtafaruku, ameweza kukiweka sawa na kucheza vizuri.
Deschamps atakuwa mtu wa tatu kuweza kushinda kombe la dunia akiwa mchezaji na kocha, alikuwa nahodha wa timu ya taifa ya Ufaransa iliyobeba kombe la dunia mwaka 1998.
Kikosi chake cha timu ya taifa ya Ufaransa, kikiongozwa na mshambuliaji wenye umri wa miaka 19 Kylian Mbappe pamoja na mchezaji mwenye uzoefu zaidi Antoine Griezmann, wanapigiwa upatu kushinda.
Paul Pogba hatimaye amekuwa kiongozi katika sehemu ya kati kwa Ufaransa na N'Golo Kante ametimiza wajibu wake kwa kufanyakazi bila kuchoka hali ambayo inawaruhusu wenzake kung'ara, huku Samuel Umtiti na Raphael Varane ni kitovu cha ngome imara.
Les Bleus
Les Bleus walikuwa na kibarua kigumu kupita katika awamu ya makundi, wakiiangusha Australia na Peru kwa bao moja tu na kutoka sare na Denmark katika pambano pekee ambalo lilitoka sare bila ya wavu kutikiswa katika mashindano haya.
Na ghalfa kikosi hicho kikaanza kucheza vizuri, kikiiweka kando Argentina katika mchezo ambao ulimtangaza duniani mshambuliaji Kylian Mbappe kwamba yuko tayari kuingia katika jukwaa la nyota wa kimataifa wakati alipopachika mabao mawili na kumfunika Lionel Messi.
Lakini licha ya ushindi wa mabao 4-3, Ufaransa ilicheza kama kikosi cha Deschamps, kikiwa na msisitizo mkubwa katika ulinzi.
Uwanja wa Luzhniki wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 80,000 utakuwa ndio jukwaa la fainali hii, lakini sherehe kubwa zaidi zitafanyika mitaani katika nchi itakayoshinda.
Mamia kwa maelfu ya watu walimiminika katika mtaa wa Champs-Elysee mjini Paris baada ya ushindi wa Ufaransa katika nusu fainali dhidi ya Ubelgiji na matumaini nyumbani yako juu.
Croatia imeonesha uwezo wa kupambana zaidi na kuhimili michezo mitatu ambayo imekwenda katika dakika za nyongeza, bao la ushindi la Mario Mandzukic katika dakika ya 109 lilitosha kuwaangusha England katika nusu fainali siku ya Jumatano.
Kocha Dalic amesema yuko tayari kufanya mabadiliko kwa ajili ya fainali iwapo wachezaji wake watashindwa kurejea katika hali ya kawaida kutokana na majeruhi.
Jana Jumamosi(14.07.2018) Ubelgiji ilifanikiwa kuchukua nafasi ya tatu katika fainali hizi za kombe la dunia kwa kuiangusha tena England kwa mabao 2-0.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi