Kombe la dunia la Kandanda kwa wanawake:Nane zaingia robofainali
7 Julai 2011Timu hizo zilizofuzu, ni pamoja na wenyeji ambao pia ni mabingwa watetezi Ujerumani, Ufaransa,Japan, Sweden, Australia, Brazil,Marekani na Uingereza.
Wawakilishi wa Afrika Nigeria na Guinea ya Ikweta wametupwa nje,Nigeria iliyokuwa katika kundi A imeshika nafasi ya tatu na kuziachia Ujerumani na Ufaransa zikisonga mbele, huku Guinea ya Ikweta ikikamata nanga katika kundi lake la D ambalo limetoa timu za Brazil na Australia.
Hali hiyo imewasononesha washabiki wa soka barani Afrika ambao wengi wao walikuwa na matumaini na timu ya Nigeria.
Katika hatua nyingine wachezaji wawili wa Korea Kaskazini wamesimamishwa kufuatia kubainika kuwa walitumia dawa za kuongeza nguvu ambazo haziruhusiwi michezoni.Uchunguzi huo ulifanyika mara baada ya mechi kati ya timu hiyo na Colombia ambapo timu hizo zilitoka suluhu bin suluhu.
Shirikisho la kandanda duniani FIFA limewataja wachezaji hao kuwa Jong Sun Song and Sim Pok Jong.Jumanne wiki hii FIFA ilitangaza kwa mlinda mlango wa Colombia Yineth Varon amepatikana na kosa la kutumia dawa hizo na hivyo kusimamishwa.
Robofainali ya michuano hiyo itaanza kesho ambapo mabingwa watetezi Ujerumani wataingiliana na Japan huko Wolfsburg, huku Uingereza ikipepetana na Ufaransa mjini Leverkusen.Jumapili itashuhudia Sweden ikicheza na Australia mjini Augsburg, ilhali Brazil itajaribu kuwacheza samba Marekani huko Dresden.
Mwandishi:Aboubakary Liongo/Reuters/DPA
Mhariri:Saumu Mwasimba