Kombe la dunia kwa wanawake Ufaransa yaanza vizuri
8 Juni 2019Wendie Renard akiwa mchezaji mrefu kabisa katika mashindano haya ya kombe la dunia kwa wanawake yanayofanyika nchini Ufaransa, alipachika mabao mawili kwa kichwa kupitia mpira wa kona, na kikosi hicho cha Les Bleues kiliwakndamiza Korea ya kusini jana Ijumaa kwa mabao 4-0 katika tamasha la ufunguzi wa kombe la dunia.
Eugenie Le Sommer na Amandine Henry pia walipachika mabao katika mchezo uliofanyika katika uwanja wa mjini Paris wa Parc des Princes, nyumbani kwa klabu maarufu ya mjini Paris , Üaris Saint-Germain.
Mwanamuziki nyota wa mitindo ya Pop Jain alihusika katika sehemu ya burudani kwa mashabiki 45,261, walioujaza uwanja huo , na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alikuwa miongoni mwa watazamaji wakiimba wimbo wa taifa "La Marseillaise".
Tulijua kwamba utakuwa usiku wa hamasa kubwa . "Lakini nafikiri tuliutayarisha vizuri," Renard alisema. "Wakati ukiwa na zaidi ya watu 45,000 wakiimba wimbo wa taifa wa Ufaransa, bila shaka unakuwezesha kupambana."
Ufaransa ni mwenyeji wa mashindano hayo katika wakati ambao timu za wanawake zinaongeza msukumo wao kwa kutendewa haki kama wengine na shirikisho la kandanda duniani FIFA pamoja na mashirika mengine yanayohusika na mchezo wa kandanda.
Taifa la kwanza kunyakua vikombe vyote vya dunia
Ufaransa linajaribu kuwa taifa la kwanza kunyakua mataji yote ya wanaume na wanawake katika kombe la dunia katika wakati mmoja.
Nina hakika watu wanamatarajio, ama matumaini, na hata sisi ni hivyo hivyo, tungependa kufuata katika nyazo za timu ya wanaume ya taifa," kocha wa Ufaransa Corinne Diancre amesema. "Lakini kila kitu kinahitaji muda. Tumeshinda usiku wa leo , lakini bado hatujashinda kitu. Tunahitaji kuwa makini na kuwa na malengo katika michezo sita, na hapo ndio tutaona kile kitakachokuja."
Norway na Nigeria zinakutana katika kundi A la ufunguzi leo Jumamosi (08.06.2019).
Ufaransa inakumbana na Norway siku ya Jumatano na wana miadi na Nigeria Juni 17.
Wigo wa ushindi wa Ufaransa ni mkubwa katika mchezo wa ufunguzi wa mashindano ya kombe la dunia la wanawake tangu pale China ilipoishinda Norway kwa kiwango hicho hicho cha mabao katika mashindano ya kwanza mwaka 1991.
Miaka minne iliyopita, timu zote tisa ambazo zilishinda michezo yake ya ufunguzi zilifika kutoka katika timu 24 za awamu ya makundi hadi katika duru ya timu 16 bora.
Timu ya nne kwa ubora duniani haikusumbuliwa kabisa na namba 14 duniani ya Korea kusini. Ufaransa ilikuwa imevurumusha mikwaju 17 -0 katika kipindi cha kwanza na ikatandika mashuti 21-4 kwa jumla katika mchezo mzima. Hii ina maana Korea kusini ilielekeza mikwaju 4 tu langoni mwa Ufaransa katika mchezo wote jana usiku.
Jioni ya leo (08.06.2019) timu ya Ujerumani itafungua dimba la kundi B kwa kupambana na China , na kisha Uhispania itakwaana na Afrika kusini.