1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kolon. Siku ya vijana wa Kikatoliki mjini Kolon.

20 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CEjA

Kiongozi wa kanisa Katoliki , Pope Benedict wa 16 ambaye yuko mjini Kolon, Ujerumani akihudhuria sherehe za siku ya vijana wa Kikatoliki duniani , amekutana na kansela Gerhard Schröder.

Kiongozi huyo wa kidini pia amezungumza na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Ujerumani Angela Merkel na rais wa bunge la Ujerumani Wolfgang Thierse kwa muda mfupi katika makaazi ya askofu mkuu wa Kolon.

Pia anatarajiwa kukutana na viongozi wa jamii ya Waislamu kutoka Uturuki wanaoishi nchini Ujerumani.

Jana Ijumaa , Pope Benedict, ambaye ni kiongozi wa kwanza wa kanisa hilo katika ngazi hiyo raia wa Ujerumani, katika karibu miaka 500, alifanya ziara ya kihistoria katika Sinagogi mjini humo.

Hiyo ilikuwa ziara ya pili ya aina yake kufanywa na Pope katika nyumba ya ibada ya Wayahudi.

Akitoa hotuba yake kwa jumuiya ya Kiyahudi, Pope Benedict alishutumu mauaji ya maangamizi yaliyofanywa na utawala wa Kinazi nchini Ujerumani wakati wa vita vikuu vya pili vya dunia, na kuonya juu ya kurejea tena chuki dhidi ya Wayahudi.

Siku ya vijana wa Kikatoliki duniani inafikia kilele kesho Jumapili kwa kufanya misa ya wazi ambayo inatarajiwa kuhudhuriwa na wazu karibu milioni moja.