1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kodi ya Mshikamano ya kuikarabati Ujerumani ya Mashariki

3 Novemba 2009

Majimbo mapya ya iliyokuwa Ujerumani Mashariki yakarabatiwa upya.

https://p.dw.com/p/KIKH
Majengo yakarabatiwa Ujerumani MasharikiPicha: AP

Baada ya kuangushwa kwa ukuta wa Berlin, Helmut Kohl ambae wakati huo alikuwa kansela wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani alitoa ahadi kuwa majimbo mapya yatafanyiwa ukarabati na kupewa sura mpya. Je pesa za kugharimia miradi ya Ujerumani iliyoungana tena zitatoka wapi? Jawabu ni kodi ya mshikamano.

Ni mabilioni ya pesa zilizohitajiwa kutekeleza kazi za ukarabati katika mashariki ya Ujerumani. Kwa hivyo pakaanzishwa kodi ya mshikamano kwa azma ya kuyasaidia majimbo mapya. Kwa ufupi kodi hiyo ni maarufu kwa jina "Soli." Kodi hiyo inalipwa na kila mwananchi kwa kukatwa kiwango fulani cha mshahara, faida ya biashara na kodi ya mashirika. Kiwango kilichokuwa kikitozwa tangu mwaka 1991 ni kati ya asilimia 7 .5 na 5.5 ya pato. Hadi hii leo zaidi ya Euro bilioni 1,000 zimemiminwa katika ujenzi wa barabara,shule na miradi ya kuvutia biashara katika majimbo hayo mapya. Lakini sehemu kubwa ya kodi hiyo ya "Soli" imetumiwa kutoa msaada kwa wakosa ajira, kuwalipa wastaafu na kusimamia miradi husika.

Lakini kodi hiyo ingali ikipingwa kisheria.Si kwa sababu tu kuwa kila raia anapaswa kulipa kodi hiyo hadi mwaka 2019. Jumuiya ya walipa kodi imejaribu mara kadhaa kushstaki mahakamani kwani pesa zinazokusanywa kwa kodi hiyo ya "Soli" hazitengwi kwa mradi maalum bali hutiwa katika mfuko mmoja wa gharama zinazosimamiwa na bajeti ya serikali. Licha ya mabilioni ya pesa zilizochangwa, wakaazi wengi katika mashariki ya Ujerumani wangali wakingojea kuona maendeleo waliyoahidiwa na kansela wa zamani Helmut Kohl baada ya muungano. Ukweli wa mambo ni kwamba idadi ya wakosa ajira ni kubwa sana, watu wanaendelea kuyahama majimbo hayo ya mashariki na wala hakuna dalili ya biashara inayokua na inayoweza kujitegemea. Hata uzalishaji wa bidhaa kwenye viwanda vya majimbo mapya unadorora kulinganishwa na viwanda vya magharibi.

Helmut Kohl
Kansela wa zamani Helmut KohlPicha: AP

Suala jingine linalozusha ubishi hadi hii leo juu ya uamuzi uliopitishwa na serikali ya Kohl linahusika na mabilioni pia. Kati ya mwaka 1945 na 1949, katika ardhi iliyokaliwa na Soviet Union, mashamba ya wamiliki ardhi na serikali ya kizalendo ya wakati huo yalitaifishwa. Ardhi hiyo ikagaiwa miongoni mwa wakulima wapya na baadae kwa nguvu ikafanywa mali ya DDR. Katika mwaka 1990 makubaliano ya muungano wa Ujerumani yalipatikana kati ya Kohl na Soviet Union kwa sharti moja. Mageuzi ya umiliki wa ardhi yasiguswe baada ya muungano. Hata wamiliki au warithi wa ardhi hizo hawatolipwa fidia baada ya kuanguka kwa ukuta. Hiyo ilikuwa mali ya serikali ya DDR na sasa ni mali ya Shrikisho la Jamhuri ya Ujerumani itakayosaidia kulipia gharama za muungano. Kohl aliamini kuwa hivyo, muungano wa Ujerumani hautowagharimu wananchi hata senti moja - kinyume na mpinzani wake Lafontaine aliekwishatamka tangu hapo awali juu ya uwezekano wa kuzuka gharama hizo kubwa.

Mwandishi: Marek,Michael/ZPR/P.Martin

Mhariri: M.Abdul-Rahman