Kocha wa Ujerumani aanza maandalizi ya kombe la Euro 2012
28 Desemba 2011Tuanzie hapa Ujerumani : wakati ikisalia miezi sita kabla ya michuano ya fainali za kuwania ubingwa wa mataifa ya Ulaya, Euro 2012 michuano itakayofanyika huko Poland na Ukraine, kocha wa Ujerumani Jogi Löw anaendelea na maandalizi ya fainali hizo, licha ya kuwa kwa sasa ligi ya Ujerumani imo mapumzikoni. Lakini muda huu si mrefu sana , na pamoja na hayo timu ya Ijurumani itakuwa na mchezo mmoja tu wa majaribio dhidi ya Ufaransa kabla ya kuingia katika kinyang'anyiro hicho. Ni eneo gani hasa Jogi Löw analolenga kulishughulikia kwa sasa katika maandalizi ya timu yake : kocha wa Ujerumani Joachim Löw amesema .
"Tunaangalia kwa kweli wachezaji wetu. Wakati tuna mchezo mmoja tu wa kimataifa wa kujipima nguvu, ni kawaida kwamba inabidi uangalie wachezaji wako katika vilabu, hususan katika mapambano yao. Jicho pia tunatupia kwa wapinzani wetu , kwa hiyo utakapoanza mwezi wa Januari tutaongeza kasi ya kuzichunguza Ureno, Uholanzi na Denmark, na tutajishughulisha zaidi pia na wachezaji mmoja mmoja, ambapo tutasema , tufanye nini ili kuwafanya wachezaji mmoja mmoja kuwa bora zaidi, tutatawapa nini cha zaidi wachezaji wetu katika kusakata soka, na kati gani muhimu tunayopaswa kuifanya katika wiki za maandalizi, ili tuweze katika kinyang'anyoro hiki kufanya vizuri, na kuweka kiwango cha soka yetu juu" .
Kocha wa Ujerumani Joachim Löw akijibu swali kuhusu ni maandalizi gani anayoyafanya kabla ya kuingia viwanjani mwezi wa Juni katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Ulaya , euro 2012.
Wakati huo huo mchezaji nyota chipukizi wa Ujerumani na Borussia Dortmund Mario Goetze anashauku kubwa na michuano hiyo ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya nchini Poland na Ukraine. Goetze , ambaye amecheza mchezo wake wa kwanza wa kimataifa na timu ya taifa ya Ujerumani dhidi ya Sweden Novemba mwaka huu , amesema jana kuwa anashauku kubwa ya kuwamo katika kikosi cha kocha Joachim Löw na kushiriki katika mashindano hayo.
Hayo yatakuwa mashindano yake ya kwanza makubwa. Ujerumani itakwaana na Ureno, Uholanzi na Denmark katika kundi B katika mashindano hayo.
Na bado tukiwa katika soka la Ujerumani Schalke 04 imepata huduma ya mshambuliaji kutoka Nigeria Chinedu Obasi kwa mkopo kutoka Hoffenheim pia ya Ujerumani , hadi utakapomalizika msimu huu , lakini kwa masharti kuwa inawezekana kurefusha mkataba huo , iwapo Schalke watapendezwa na huduma ya Obasi.
Mshambuliaji huyo anamkataba na Hoffenheim hadi mwaka 2014, tangu mwaka 2007. Mchezaji huyo wa Nigeria ameichezea Hoffenheim mara 65 na kufunga mabao 13 lakini kwa hivi sasa amepoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha Hoffenheim.
Katika Premier league sasa, Meneja wa zamani wa Chelsea Jose Mourinho ana lengo la kurejea katika Premier League atakapomaliza muda wake katika klabu ya Real Madrid, amesema hayo leo Jumatatu. Nina furaha sana kuwapo Madrid , Mourinho amesema katika kipindi cha radio 4 cha BBC cha "Today". Sikutaka kupoteza fursa ya kufanyakazi hapa lakini shauku yangu ni Uingereza na hatua yangu ijayo itakuwa kurejea huko, iwapo itawezekana, na nikiwa huko nitakaa kwa muda mrefu, amesema Mourinho, ambaye mkataba wake wa miaka minne na Real unamalizika mwishoni mwa msimu wa 2013-14. Kipindi chake cha miaka mitatu na Chelsea kilimalizika mwaka 2007 na alikwenda Italia akaiongoza Inter Milan hadi ubingwa wa champions League, ikiwa ni ubingwa wake wa pili wa kombe hilo kufuatia ule wa mwaka 2004 akiwa na FC Porto.
Nae meneja wa Arsenal Arsene Wenger anakiri kuwa ratiba ya michezo ya Premier League katika wakati huu wa siku kuu ya Chrismas ambapo timu hiyo inaumana na Wolves, Qeens Park Rangers na Fulham inaweza kutoa picha ya msimu huu kwa timu hiyo. Arsenal ambayo inapambana na Wolves kesho Jumanne , iko points mbili tu mbele ya Liverpool ambayo iko nafasi ya sita , lakini iko points moja tu nyuma ya timu iliyoko nafasi ya nne Chelsea.
Wenger amesema kuwa anafahamu kuwa timu yake ina nafasi ya kujisogeza juu zaidi ya msimamo wa ligi . Na akaongeza, Ni wajibu wetu kufanyakazi hiyo.
Wakati huo huo , Wenger anaamini bahati yake ya kupata mchezaji wa nafasi ya ulinzi wa kushoto inawasi wasi , lakini hajatoa ombi lolote la kupata mtu atakayeshikilia nafasi hiyo kwa muda. Wenger alibaki bila ya kuwa na mchezaji halisi ya nafasi hiyo ya ulinzi wa kushoto baada ya Kieran Gibbs kufanyiwa upasuaji katika paja Alhamis wiki iliyopita. Gibbs anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa mwezi mmoja na anajiunga na mchezaji mwenzake wa nafasi hiyo Sandro Santos ambaye naye ameumia.
Cesc Fabregas wa Barcelona amesema jana kuwa ana matumaini ya kumaliza muda wake wa kucheza soka na Barcelona, lakini iwapo ataondoa katika timu hiyo kigogo cha soka la Uhispania atarejea tu Arsenal London na sio kwingineko. Mbali ya Arsenal na Barcelona sioni timu nyingine ambayo naweza kuichezea , amsema mchezaji huyo wa kiungo mwenye umri wa miaka 24. Wakati nikiwa na nafasi ya kuangalia mchezo nakwenda Arsenal , kukutana na mafariki na mashabiki , na huwezi kujua hapo baadaye naweza kurejea Arsenal.
Nina matumaini kuwa nitabakia hapa kwa muda mrefu , na hata kustaafu , lakini nani anajua , katika maisha huwezi kusema haiwezekani. Na kama kuna sehemu nyingine naweza kwenda , ni Arsenal , hiyo ni hakika amesema Frabregas.
Naye mchezaji wa kiungo wa Barcelona Seydou Keita ameteuliwa jana Jumapili kuwa mchezaji bora wa mwaka 2011 nchini Mali. Keita ambaye atakuwa miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Mali katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Afrika mwezi ujao, ameisaidia Barcelona kunyakua taji la ubingwa wa Ulaya Champions League , ligi ya Uhispania, La Liga, na kombe la dunia la vilabu hivi karibuni nchini Qatar.
Mchezaji wa Tottenham Hot Spurs Emmanuel Adebayor anaamini kuwa msukumo wa timu ya Manchester City kuwania kunyakua ubingwa wa ligi msimu huu unaweza kuingia matatani kutokana na mashindano ya kombe la mataifa a Afrika mwakani. City watakosa huduma ya ndugu wawili muhimu katika kikosi hicho yaya Toure na Kolo Toure ambao watajiunga na kikosi cha Cote D'Ivoire kwa ajili ya michuano hiyo inayoanza Januari 21 hadi February 12, wakati Spurs haitaathirika kwa kuwa Togo ambako Adebayor anatoka imepigwa marufuku kushiriki mashindano hayo.
Adebayor amesema kuwa City ni timu nzuri, yenye ari kubwa na kwa wakati huu inacheza soka safi kabisa , lakini wakipata majeruhi wachache , nafikiri itakuwa vigumu sana kwao.
Sir Alex Ferguson amekataa wazo la kutokuwepo na changamoto kubwa kutoka mjini London kileleni mwa msimamo wa ligi ya Uingereza Premier League mwakani licha ya timu mbili za mjini Manchester kutamalaki . Uwezo mkubwa ulioonyeshwa na Manchester United na viongozi wa ligi hiyo kwa sasa Manchester City umesababisha wadadisi wengi wa mambo ya soka kuamini kuwa bingwa atatoka katika mji wa Manchester. Hata hivyo , licha ya kuwa Tottenham iliyo katika nafasi ya tatu kwa sasa iko nyuma kwa points saba nyuma ya Manchester United , lakini kikosi cha kocha Harry Redknapp kina mchezo mmoja zaidi na historia imemfunza kocha wa siku nyingi wa Manchester United kuwa changamoto dhidi ya nia yao ya kulinyakua tena taji hilo inaweza kutoka katika vyanzo mbali mbali katika mwaka mpya.
Na huko nchini Hispania , mshambuliaji wa Barcelona David Villa ametoka hospitalini siku tano baada ya kufanyiwa operesheni katika mguu wake uliovunjika wakati wa michuano ya kombe la dunia la vilabu nchini Qatar.
Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Hispania, Villa bingwa wa dunia na kombe la champions League, anatarajiwa kubakia nje ya uwanja hadi miezi mitano, na kwamba ushiriki wake katika kombe la mataifa ya Ulaya euro 2012 uko mashakani.
Watu wenye ulemavu watapatiwa tiketi za bure 32,000 kuingia katika michezo ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil. Hayo yamesemwa na chama cha mpira wa miguu nchini Brazil ambacho kimetoa bure tiketi hizo, ambapo zitagaiwa kwa mpango wa tikiti 500 kwa kila mchezo. Gharama itakuwa kiasi cha euro milioni 10. Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil Ronaldo amesema.
"Mara nyingi wenye ulemavu huwa hawafikiriwi katika mashindano kama haya . Tunataka kubadilisha hali hiyo. Hatuwasahau watu wenye ulemavu."
Mshambuliaji wa zamani wa Brazil ambaye alikuwa bingwa wa dunia katika kikosi cha Brazil mwaka 1994, Romario ambaye ni mbunge katika bunge la Brazil tangu mwaka 2010 ameamua kuchangia sehemu ya tiketi hizo za bure kwa walemavu.
Mwandishi : Sekione Kitojo / ZR / afpe /dpae
Mhariri: Othman Miraj