1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kobler ziarani Tripoli kwa mara ya kwanza

5 Aprili 2016

Mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya amekutana na waziri mkuu mpya pamoja na maafisa wa baraza la uatawala la Libya katika juhudi za kuleta amani na utulivu katika nchi hiyo iliyovurugwa na vita

https://p.dw.com/p/1IPoV
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Libya Martin Kobler
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Libya Martin KoblerPicha: picture alliance/AA/A. Landoulsi

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Libya amekutana na serikali mpya ya umoja wa kitaifa akiwa katika ziara yake ya kwanza katika nchi hiyo iliyogubikwa na vita tangu waziri mkuu mteule Fayez al-Sarraj alipowasili katika mkuu wa nchi hiyo Tripolisi wiki iliyopita. Martin Kobler ameingia Tripoli katika wakati ambapo Jumuiya ya Kimataifa imejenga matumaini kwamba utawala mpya wa waziri mkuu Sarraj utaweza kuidhibiti hali katika nchi hiyo na kumaliza vurugu ambazo zinaikabili Libya tangu Moammer Ghaddafi alipoangushwa madarakani na kuuwawa mwaka 2011.

Martin Kobler amefahamisha kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba kwa hivi sasa anakutana na waziri mkuu Sarraj pamoja na maafisa wa baraza la utawala na anafurahia kuwepo kwake Libya na hatua ya kuingia katika majadiliano kuhusu mustakabali wa taifa hilo.

Kobler ambaye ni raia wa Ujerumani ni mwanadiplomasia aliyeteuliwa mwaka jana kuongoza juhudi za Kimataifa kuutatua mgogoro wa Libya na ameweka picha zinazomuonesha yeye akiteremka kwenye ndege ya Umoja wa Mataifa na baadae kukutana na maafisa wa Libya akiwemo waziri mkuu Sarraj. Kimsingi mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya mnamo mwezi uliopita alizuiwa kusafiri kuelekea mji mkuu Tripoli na maafisa wanaoudhibiti mji huo ambao hadi sasa wamekataa kuachia madaraka ya mji huo kwa serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Tangu ulipoangushwa madarakani utawala wa kanali Muamar Ghaddafi Libya imekuwa na serikali mbili zinazopingana. Serikali inayotambuliwa kimataifa ililazimika kuondoka mjini Tripoli katika ya mwaka 2014 na kukimbilia Mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuzuka vurugu na vita vikali vya kuwania madaraka.

Martin Kobler akiwa katika mkutano na waandishi habari mwaka 2015 Libya
Martin Kobler akiwa katika mkutano na waandishi habari mwaka 2015 LibyaPicha: picture alliance / dpa

Serikali ya umoja wa Kitaifa imeundwa chini ya makubaliano ya kugawana madarakana na baadhi ya wabunge mnamo mwezi Desemba. Kutokana hata hivyo na hali ya usalama kutokuwa ya kuaminika kwa kiasi kikubwa waziri mkuu mpya Sarraj aliwasili toka Jumatano wiki iliyopita kwa njia ya baharini na toka wakati huo amekuwa akiendesha shughuli zake katika kambi ya jeshi la majini.

Utawala mpya wa Libya umefanikiwa kutanua uungaji mkono ambapo umekubalika hata na shirika la uwekezaji la Libya pamoja na shirika la taifa la mafuta na benki kuu ya taifa hilo.Serikali za nchi za Magharibi zina wasiwasi kwa kiasi kikubwa kwamba mvutano wa Libya umetoa nafasi kwa kundi la kigaidi la dola la kiislamu IS kujiimarisha katika nchi hiyo lakini vile vile nchi hizo zimesema nchi za kigeni zinaweza tu kuingilia kati hali ya taifa hilo pale tu serikali ya Umoja wa Kitaifa itakapotoa ombi hilo.

Mhariri: Daniel Gakuba