1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Klose aiokoa Ujerumani

22 Juni 2014

Baada ya kuirarua Ureno kwa mabao 4-0 katika mchezo wa ufunguzi, Ujerumani ilionekana kama itapata mteremko dhidi ya Ghana wakati Mario Goetze alipopachika bao la kuongoza katika dakika ya 51 ya mchezo mjini Fortaleza.

https://p.dw.com/p/1CNlT
WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Miroslav Klose akishangiria bao la kusawazisha la UjerumaniPicha: Getty Images

Lakini Ghana walizinduka na kupachika mabao mawili ambayo ilihitaji ujuzi usio zeeka wa Miro Klose kuiokoa Ujerumani katika ukingo wa kushindwa.

Ujerumani ilirejesha bao katika dakika ya 71 ya mchezo kwa bao la mchezaji huyo wa akiba Miroslav Klose, baada ya Ghana kupachika mabao wawili ambapo Andre Ayew alikwamisha mpira wavuni kwa kichwa pamoja na pasi safi kutoka kwa Sulley Muntari iliyomuweka Asamoah Gyan katika nafasi ya kupachika bao la pili kwa Ghana.

WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Mpambano wa ndugu wawili Boateng Prince wa Ghana na Boateng Jerome wa UjerumaniPicha: Reuters

Ujerumani ina points 4, Marekani ikiwa na points tatu , Ghana ina point moja na Ureno haina kitu kabla ya mchezo wake dhidi ya Marekani leo Jumapili(22.06.2014) katika kundi hilo la G.

Klose aifikia rekodi ya Ronaldo

Klose ameshiriki michezo 20 ya kombe la dunia kwa Ujerumani na amepachika mabao 15 na sio jambo baya kabisa , kocha wa Ujerumani Joachim Loew ameiambia televisheni ya Ujerumani.

WM 2014 Gruppe G 2. Spieltag Deutschland Ghana
Andre Ayew akishangiria bao la kusawazisha la GhanaPicha: Reuters

"Lakini kitu muhimu ni kwamba tutakuwa na mchezo mzuri dhidi ya Marekani, " ameongeza.

Goli la Klose dhidi ya Ghana pia limemsogeza karibu na orodha ya mabao aliyoweka wavuni mchezaji wa zamani wa Ujerumani Gerd Mueller, ambaye aliiongoza Ujerumani magharibi wakati ule katika ubingwa wa dunia mwaka 1974.

Nigeria yazinduka

Nigeria nayo jana (21.06.2014) ilifanikiwa kuiangusha Bosnia Herzegovina kwa bao 1-0 na kuandika ushindi wao wa kwanza katika kombe la dunia tangu mwaka 1998 na kuitupa kando timu hiyo kutoka bara la Ulaya na kujiunga na timu kadha za bara hilo zinazoyaaga mashindano haya na mapema , Bosnia ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki katika fainali za kombe la dunia na kuondoka na mapema.

WM 2014 Gruppe F 2. Spieltag Argentinien Iran
Lionel Messi amewaliza WairanPicha: Juan Mabromata/AFP/Getty Images

Goli la Peter Odemwingie katika dakika ya 29 lilitosha kuwanyanyua mabingwa hao wa bara la Afrika kufikia points 4 katika michezo miwili, ikiwa nyuma ya Argentina ambayo inakutana nayo katika mchezo wa mwisho wa kundi F, siku ya Jumatano .

Ni miaka 16 na hatujaipatia nchi yetu ushindi kwa hiyo tumefurahi mno," Odemwingie amesema katika mahojiano katika televisheni.

"Tunahitaji kushinda. Wana wachezaji wazuri kwa hiyo tumefurahi kurejea tena baada ya kile watu nchini mwetu walichokuwa wakifikiri kuwa ni mchezo mbovu tuliocheza katika mchezo wa kwanza na Iran," ameongeza Odemwingie.

WM 2014 Gruppe F 2. Spieltag Argentinien Iran
Ashkan Dejagah akitoka njePicha: Getty Images

Katika mchezo wa kwanza jana (21.06.2014) Argentina nahodha wa kikosi hicho Lionel Messi ameiokoa timu yake kwa kupachika bao safi katika fainali hizi za kombe la dunia nchini Brazil.Messi alipachika bao hilo katika dakika za majeruhi na kusababisha pigo kubwa kwa Iran ambayo mara kadhaa ilifikia karibu ya kupata bao la kuongoza.

Bao hilo limetosha kuiwezesha Argentina kukata tikiti yake katika timu 16 bora kutoka kundi F wakati ikiwa na mchezo mmoja kibindoni.

"Unapokuwa na Messi kila kitu kinawezekana," kocha wa Argentina Alejandro Sabella amewaambia waandishi habari.

"Hata wangekuwa walinda mlango wawili hawangeweza kuzuwia mkwaju ule wa Messi," ameongeza Alejandro.

Mapambano yanaendelea

Leo(22.06.2014) Ubelgiji itapambana na Urusi, wakati Korea ya kusini ina miadi na Algeria katika michezo ya kundi H, wakati Marekani inaisubiri Ureno katika mchezo wa kundi G, ambapo kocha Paulo Bento amesema kikosi chake kinaweza kuanza kufungasha virago iwapo hakitafanikiwa kuiangusha Marekani mjini Manaus.

Bildergalerie Schönste Fußballer Cristiano Ronaldo
Cristiano Ronaldo wa UrenoPicha: Lars Baron/Bongarts/Getty Images

Ureno ilikandikwa mabao 4-0 na Ujerumani katika mchezo wa ufunguzi wa kundi G na bila kushinda leo dhidi ya Marekani hali itakuwa ngumu kuweza kukata tikiti kuingia katika awamu ya mtoano ya timu 16 bora zitakazoendelea katika fainali hizi nchini Brazil.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre

Mhariri: Sudi Mnette