Kizazi njia panda - awamu ya nne
3 Juni 2015Matatizo yanayomkumba Mercy ni mengi mno. Analazimika kuugawa muda wake kama Mama na mke nyumbani kwa upande mmoja na upande mwingine kuendelea kuzingatia masomo yake ya Chuo Kikuu na pia mfanyakazi katika kituo cha redio chuoni anakosemea. Mbali na hayo bado kuna tatizo la kumsaidia mumewe, Niki Jumbe baada ya kufahamu kwamba ameathirika na virusi vya Ukimwi. Lakini maajabu hayakosi maishani.
Dan bado anaendelea na kampeni yake ya kulinda mazingira na anaanzisha mradi mpya. Kupitia kipindi chake cha redio Tina anakubali kumsaidia Dan katika kampeni yake, na kisha baadae anakuja kufahamu kwamba, Dan ni zaidi ya rafiki wa kawaida. Lakini je, Dan anahisi mahaba aliyonayo Tina? Anita pia anarejea Kisimba na anafurahia sana kazi anayofanya ya kuisaidia jamii. Je, ataweza kumsaidia Noni msichana mlemavu anayefichwa na wazazi wake kwa kufungwa minyororo mchana kutwa nyumbani kwao?
Mambo yanabadilika baada ya mkasa wa mafuriko kuikumba Kisimba. Nusra ndoa ya Niki na Mercy ivunjike, na upande mwingine Lulu naye apoteza biashara yake huku wanawe wawili Kadu na Banda wakikabiliwa na kitisho cha ugonjwa wa homa ya matumbo. Kwa wengine, mkasa huo wa mafuriko unakuwa na maafa makubwa. Ingawa washiriki wote kwenye mchezo huu wanajaribu kuanza kujenga upya maisha yao. Kwa hakika mchezo huu wa Kizazi Njia Panda unaashiria maudhui halisi kwamba “Maisha Yamo Mikononi Mwetu”.