Kiwingu mazungumzo ya Yemen
7 Desemba 2018Wawakilishi wa serikali ya Yemen na waasi wa Houthi walio kwenye uhasama mkubwa walishambuliana kwa maneno jana alhamisi wakati wa siku ya kwanza ya mazungumzo yaliyofikiwa kwa tabu na Umoja wa Mataifa ambao umeyataja kuwa magumu lakini yenye umuhimu.
Mazungumzo ya nchini Sweden baina ya pande hizo mbili ni ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili iliyopita juu ya mzozo ambao umeitumbukiza Yemen, taifa masikini la Kiarabu kwenye baa kubwa la njaa na hali mbaya kabisa ya kibinadamu.
Siku ya kwanza ya mazungumzo ya Sweden ilitawaliwa zaidi na kila upande kutaka masharti yake yazingatiwwe kwa umakini na kupewa kipaumbele.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizitolea wito pande zote mbili kutoweka masharti kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo yanayofanyika kwenye kitongoji kidogo cha Rimbo kaskazini ya mji mkuu wa Sweden, Stockholm, yatakayodumu kwa muda wa wiki moja.
Safari bado ni ndefu kufikia amani
Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye mzozo wa Yemen Martin Griffiths amesema mazungumzo hayo yametoa nafasi muhimu lakini alijizuia kufafanua kuwa ni awamu ngapi za mazungumzo zitahitajika kabla ya kufikia mwisho wa uhasama kati ya serikali na waasi wa Houthi.
Hata hivyo upande wa waasi umesema una wasiwasi juu ya dhamira ya mazungumzo hayo na kuwa wa bado unatathmini umuhimu wa kuendelea kushiriki.
Msemaji wa waasi wa Houthi Mohammed Abdelsalam alikiambia kituo kimoja cha televisheni kuwa wataamua leo ijumaa ikiwa mazungumzo ya Stockholm yana nia ya dhati ya kumaliza mzozo uliopo au la.
Mazungumzo ya Sweden yatatawaliwa kati siku chache zijazo na hatma ya mji wa bandari wa Hodeida ambao umekuwa kitovu cha mapigano kati ya waasi na vikosi vya serikali vinavyoungwa mkono kijeshi na muungano wa Saudi arabia.
Mapigano yanahofiwa yamesababisha kiasi raia 150,000 kukwama bila msaada wa chakula na matibabu na mjumbe wa Umoja wa Matiafa kwa Yemen amesema wanalenga kumaliza mapigano kwenye mji huo wa bandari ambao ndiyo lango la kuingiza kiasi asilimia 90 ya mahitaji yote nchini Yemen.
Waasi waliwatesa wafungwa
Wakati huo huo Shirika la habari ya assosciated press limeripoti kuwepo ushahidi kuwa waasi wa Houthi wamefanya vitendo vya ukatili na utesaji kwa wafungwa waliokuwa wakiwashikilia.
Ushahidi huo unajumuisha rikodi za utesaji na ukatili uliotendwa na waasi dhidi ya wafungwa ikiwemo kuwachapa viboko usoni, kuning´inizwa wakiwa wamefungwa Kamba sehemu za siri na kuchomwa kwa kutumia tindikali.
Zaidi ya visa 1000 vya mateso vilivyofanywa na waasi kwenye magereza ya siri ikiwemo vifo vya raia 126 vilivyotokana na unyanyasaji vimerikodiwa.
Mwandishi: Rashid Chilumba/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef