1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiwango cha maambukizi barani Afrika bado kiko chini

Sekione Kitojo
1 Aprili 2020

Katika  bara  la  Afrika , nchi  zimerekodi  zaidi  ya  kesi 5,700  za maambukizi  ya  virusi  vya  corona  na  vifo 190, kwa  mujibu wa idadi  iliyotolewa  na  shirika  la  habari  la  AFP.

https://p.dw.com/p/3aICg
Nigeria Lagos | Coronavirus | Temperaturmessung
Picha: DW/F. Facsar

Janga la virusi vya corona  limeuwa watu watano na kuwaambukiza watu wengine  zaidi ya  1,300 nchini Afrika  kusini, waziri  wa  afya wa  nchi  hiyo  amesema jana, akitoa  matumaini  kidogo kwamba usambaaji  wa  virusi  hivyo  sio wa  kasi  kama  ilivyotarajiwa. Ugonjwa wa COVID-19 tayari umeshaingia  Burundi, nchi  ambayo kwa muda  mrefu ilikuwa  haijaguswa na maambukizi  ya  virusi hivyo. Sekione Kitojo  na  taarifa  zaidi.

Südafrika Johannesburg | Ausgangssperre wegen Coronavirus
Mitaa ya mji wa Johannesburg ikiwa tupu kutokana na hatua za kuwataka wananchi wake kubakia nyumbaniPicha: Getty Images/AFP/M. Spatari

Wagonjwa  wawili wamethibitika  kuwa  na  ugonjwa  huo  wa COVID-19 , mmoja  akiingia  nchini humo  akitokea  Rwanda,  na mwingine  ni  raia wa  nchi  hiyo  ambaye  aliingia  nchini  humo akitokea  Dubai. Timu  ya  mawaziri  na  maafisa  mbali  mbali  wa serikali wanaohusika  na mapambano  dhidi ya  kuenea  kwa   virusi vya  corona  nchini  humo wanakutana  wakati huu  kujadili  hatua zaidi  za  kuchukua.

Janga  la   virusi  vya  corona  limewauwa  watu  watano  nchini Afrika  kusini na  watu 1,353  wameambukizwa  ugonjwa  huo , waziri wa  afya  Zweli Mkhize  amesema  na  kuongeza  kwamba  licha  ya uchelewesho  na  wingi  wa  sampuli  za  damu  katika huduma za maabara, watu 39,500  wamefanyiwa  uchunguzi  wa  virusi  hivyo wakati  nchi  hiyo  inaingia  katika  siku  ya  tano  kati  ya  siku 21 za kufungwa  kabisa .

Kiwango  cha  ongezeko  la  maambukizi  hakiko  juu  kama ilivyotarajiwa," Mkhize  amesema.

Lagos mitaa iko  tupu

Mji wenye  wakaazi  wengi  kabisa  barani  Afrika  wa  Lagos umekuwa  hauna watu  mitaani  baada  ya  Nigeria  kuwataka wakaazi  wake  kubakia  nyumbani  na  kuufunga  mji  huo  ambao  ni kitovu  cha  biashara nchini  humo , pamoja na  mji  mkuu  Abuja.

Nigeria Lagos | Coronavirus | Temperaturmessung
Polisi akimpatia mkaazi wa Lagos barakoa kujikinga na maambukizi ya virusi vya coronaPicha: DW/F. Facsar

Katika  bara  la  Afrika , nchi  zimerekodi  zaidi  ya  kesi 5,700  za maambukizi  ya  virusi  vya  corona  na  vifo 190, kwa  mujibu wa idadi  iliyotolewa  na  shirika  la  habari  la  AFP.

Idadi hiyo imekuwa  ya  chini  ikilinganishwa  na  mabara  mengine, na  kuna  baadhi  ya  nchi  ambazo  bado  hazijapata mtu aliyeambukizwa.

Lakini  wataalamu  wamekuwa  wakionya  kuhusu  hali tete  ya Afrika , wakieleza  kuhusu mizozo yake  mingi, ukosefu  wa maeneo ya  kufanya  usafi wa  mwili, maeneo  ya  mijini  yenye wakaazi wengi  katika  maeneo  ya  mabanda pamoja  na  hospitali  ambazo hazina  vifaa  vya  kutosha, na  kusema  kuna  uwezekano  wa kuzuka  maafa  makubwa.

Südafrika Lockdown Ausgangssperre Obdachlose
Wanajeshi wakimtaka mwanamke ambaye hana makaazi kwenda katika kituo cha kukusanyika mjini JohannesburgPicha: AFP/M. Spatari

Tanzania, Botswana  na  mauritania zimekuwa  nchi  za  hivi  karibuni kabisa  kutangaza  vifo  kutokana na  virusi  vya  corona na Sierra Leone imethibitisha  mtu wa kwanza  kuambukizwa.

Ethiopia  imetangaza  kuahirisha  uchaguzi  wa  bunge  uliopangwa kufanyika  mwezi  Agosti  mwaka  huu kutokana  na  kuzuka  kwa ugonjwa wa  corona. Uchaguzi  huo ulionekana  kama  mtihani muhimu kwa  ajenda  za  mageuzi  za  waziri  mkuu Abiy Ahmed katika  kile  ambacho  kilikuwa  hapo  kabla   taifa  lenye ukandamizaji  mkubwa  barani  Afrika.