1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo cha wagonjwa wa Ebola chachomwa DRC

25 Februari 2019

Wakaazi wa Butembo, Kivu ya Kaskazini katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wameamka na butwaa alfajiri ya leo, baada ya kituo kinachowahifadhi wagonjwa wa Ebola cha Katwa kuchomwa moto na watu wasiojulikana.

https://p.dw.com/p/3E2Ds
Kongo Beni - Gesundheitspresonal mit Schutzanzug bei Ebola Behandlungszentrum
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. K. Maliro

Mashambulizi hayo yanahofiwa yatasababisha kusambaa kwa homa ya Ebola katika maeneo kadhaa. Akizungumza na DW kwa njia ya Whatshapp, mratibu wa masuala ya afya wa wilaya ya Katwa, Dokta Mukoko Kyota, amelaani shambulio hilo huku akiwaomba wakaazi wa Butembo kujiunga na timu za matabibu katika mpango wa kukabiliana na homa ya Ebola.

Viongozi kadhaa wa serikali katika ngazi zote wamejitokeza pia kulaani kitendo cha kuchomwa moto kituo hicho wanakotibiwa wagonjwa wa Ebola. Akiwahutubia wakaazi wa Butembo kwa njia ya redio hivi leo, meya wa mji huo, Sylvain Kanyamanda, amewataka wakaazi wa Butembo kutopingana na harakati za kupambana na homa ya Ebola.

"Ebola ipo hapa na hamna aliyeleta Ebola hapa, na hali inatisha. Raia wa Butembo fungueni macho, toeni mchango wenu katika mpango wakukabiliana na ugonjwa huo. Ugonjwa huo upo hapa, msiwashambulie watu, msivishambulie vituo vinavyowapokea wagonjwa kwa ajili ya matibabu," alisema Kanyamanda.

Demokratische Republik Kongo - Wahl: Corneille Nangaa Yobeluo
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, Corneil NangaaPicha: Getty Images/AFP/L. Tato

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, CENI, Corneil Nangaa yuko ziarani katika eneo hili, kwa matayarisho ya uchaguzi wa marudio baada ya ule wa Desemba 30 mwaka jana kuahirishwa katika mji na wilaya ya Beni pamoja na mji wa kibiashara wa Butembo katika mkoa wa Kivu ya kaskazini, kutokana na kile kilichosemwa na CENI wakati huo kuwa ni kuepuka maambukizi ya virusi vya Ebola wakati wakupiga kura. Mwenyekiti huyo wa CENI pia ametumia fursa ya ziara yake hii kuwahamasisha raia dhidi ya Ebola.

"Tunatoa mchango wetu katika mpango wa kupambana na homa ya Ebola. Kwa hiyo nawakumbusheni wote kwamba ni wajibu wetu kisiasa, kijamii na kwa hali yote kutokomeza homa ya Ebola," alifafanua Nangaa.

Hata hivyo, wengi wanahofia kuwa huenda CENI ikatumia suala la kuchomwa moto kwa kituo cha afya cha Katwa mjini Butembo kama fursa ya kuahirisha mara tena uchaguzi wa wabunge katika mji na wilaya ya Beni pamoja na mji wa kibiashara wa Butembo, jambo litakalowapelekea wakaazi wa eneo hili kutochangia katika uchaguzi wa rais pamoja na gavana.

Jumla ya watu mia tano na arubaini na sita wameshafariki dunia tangu kutangazwa kwa mripuko wa homa ya Ebola katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini pamoja na mkoa jirani wa Ituri. Idadi ya maambukizi nayo inaongezeka siku baada ya siku, hasa katika maeneo yanayoshuhudia mashambulizi dhidi ya timu za matabibu wanaokabiliana na homa hiyo kali.

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Beni
Mhariri: Mohammed Khelef