1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kituo cha kijeshi cha Syria chashambuliwa

7 Septemba 2017

Jeshi la Syria limesema ndege za kivita za Israel zimeshambulia eneo lake la kijeshi katika mji wa Hama ulioko magharibi mwa nchi hiyo. Lakini Israel mpaka sasa haijatoa tamko lolote.

https://p.dw.com/p/2jUtU
Libanon Offensive gegen IS
Picha: picture-alliance/AP Photo/Lebanese Army Website

Taarifa ya jeshi la Syria imesema shambulio hilo limewauwa watu wawili na watu wengine watano walijeruhiwa na pia taarifa ya jeshi la Syria imefahamisha kuwa shambulio hilo limesababisha uharibifu wa mali katika eneo lililo karibu na mji wa Masyaf. Eneo lililopo baina ya mji wa Hama na bandari inayotumiwa na vikosi vya wanamaji vya Urusi. Jeshi la Syria limeonya juu ya hatari zinazoweza kutokea baada ya shambulio hilo ambalo imeliita ni la uchokozi wa moja kwa moja dhidi ya jeshi na ambalo linaweza kuvuruga utulivu uliopo katika jimbo la magharibi mwa Syria.

Shirika linalofuatilia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza limesema shambulio hilo lililenga kituo cha utafiti wa kisayansi ambacho Marekani inadai kuwa ni kituo kinachotengeneza silaha za kemikali.  Marekani imekuwa inalaumu kuwa kituo hicho ndicho kilichosaidia katika kutengeneza gesi ya sumu iliyosababisha mauaji ya ´watu katika mji wa Khan Sheikhun mnamo mwezi wa Aprili. Mkuu wa shirika hilo linalofuatilia ukiukaji wa haki za binadamu nchini Syria Rami Abdulrahman amesema maeneo mawili yalishambuliwa ikiwa ni kituo hicho cha utafiti wa kisayansi pamoja na kambi ya jeshi ambayo pia ni hifadhi ya silaha za masafa mafupi.

Syrien Präsident Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al AssadPicha: picture alliance/AP Photo

Shambulio hilo limefanyika wakati ambapo Israel inaadhimisha miaka kumi tangu nchi hiyo ilipokishambulia kinu cha nyuklia nchini Syria na limefanyika baada ya waangalizi wa Umoja wa Mataifa walipotangaza siku ya Jumatano kuwa serikali ya Syria ndio iliyohusika na mashambulizi ya gesi ya sumu ya mwezi April katika eneo la kaskazini mwa Syria ambapo zaidi ya watu 83 waliuwawa.

Tangu kuzuka mgogoro nchini Syria mnamo mwaka 2011, Israel imefanya mashambulio kadhaa ya angani dhidi ya wapiganani wa Hezbolah kutoka Lebanon wanaomuunga mkono rais wa Syria Bashar Al Assad katika nchi ya Syria ambayo inakumbwa na machafuko.

Israel mpaka sasa haijatoa tamko lolote lakini aliyekuwa zamani anaongoza kikosi cha upelelezi cha Israel Amos Yadlin amesema kituo hicho kimeshambuliwa kwa sababu kilikuwa kinatengeneza silaha za sumu ila hakutamka wazi kuwa ni majeshi ya Israel ndio yaliyofanya mashambulizi hayo.  Serikali ya Syria imesema haimiliki tena silaha zozote za sumu na hasa baada ya makubaliano ya mwaka 2013 pale ilipokubali yenyewe kusalimisha silaha zake za kemikali.

Mwandishi:Zainab Aziz/AFPE/RTRE/APE

Mhariri:  Yusuf Saumu