Kitisho cha wapiganaji wa IS kukimbilia Libya
5 Desemba 2015Hayo yamesemwa na waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean Yves Le Drian katika matamshi yaliyochapishwa leo Jumapili(05.12.2015).
"Tunaona wapiganaji wa jihadi kutoka ng'ambo wakiwasili katika jimbo la Syrte kaskazini mwa Libya, ambao iwapo operesheni zetu nchini Syria na Iraq zitafanikiwa kupunguza eneo linalomilikiwa na kundi la Daesh, (Dola la Kiislamu, IS) inawezekana kesho kuwa na makundi mengi," waziri wa ulinzi Jean-Yves Le Drian ameliambia jarida la kila wiki la Jean Afrique.
Le Drian ameondoa uwezekano wa kuingilia kati nchini Libya lakini ameyaonya mataifa ya magharibi kujaribu kwa kadiri ya uwezo wao kuleta umoja nchini Libya kutokana na kitisho kama hicho.
Mazingira salama kwa IS
"Ni kitisho kikubwa na ndio sababu kunahitajika hali ya kuelewana miongoni mwa Walibya," amesema Le Drian.
Wachambuzi wanaamini Libya haitakuwa na mazingira salama sana kwa kundi la IS kama ilivyo kwa Syria na Iraq.
Lakini Libya inazuiwa katika kuwasilisha nguvu ya pamoja , wakati serikali hasimu nchini humo zinavutana kuwania madaraka--- ikiwa ni muungano wa wanamgambo wakiwa pamoja na makundi yenye itikadi za Kiislamu ambayo yameukamata mji mkuu Tripoli Agosti mwaka 2014, na serikali inayotambuliwa kimataifa ambayo imehamishia makaazi yake mashariki mwa Libya.
Ghasia zinazotokea hivi sasa nchini Libya wakati makundi ya wanamgambo wanaoshindana tangu kuangushwa na hatimaye kuuwawa kwa kiongozi wa Libya Mouammar Gaddafi mwaka 2011 kumetoa fursa kwa kundi la IS kujenga ushawishi wake, hususan katika mji anakotoka Gaddafi wa Sirte ulioko katika pwani, mashariki mwa mji mkuu Tripoli.
Na kuna hofu iliyotanda kwamba kundi hilo linaweza kutumia hali ya mizozo ya kikabila katika maeneo ya ndani ya bara la Afrika.
Muungano wa makundi ya Jihadi
Akitambua kuongezeka kwa maeneo yanayodhibitiwa na kundi la IS nchini Libya, Le Drian amesema anahofia kwamba hatimaye kundi hilo linaweza kuunda changamoto kubwa ya jihadi pamoja na kundi la Boko Haram, ambalo limekula kiapo cha utii kwa Waislamu wenzao wenye itikadi kali mwezi Machi na ambalo limesababisha ugaidi nchini Nigeria, Niger, Chad na Cameroon.
"Kuna kitisho kikubwa cha ushirika unaojengwa pamoja na Boko Haram," amesema Le Drian, akizitaka serikali mbili hasimu nchini Libya kufikia msimamo wa pamoja wakati akizitaka nchi jirani za Algeria na Misri kutumia njia za kidiplomasia kuweza kufikiwa muafaka.
Lakini Le Dran amesisitiza kwamba Ufaransa haina fikira za kuchukua hatua za kijeshi kwa hivi sasa ambapo Walibya wamegawika.
"Hilo si suala linalotushughulisha. Hatuwezi kuwaondoa Walibya kutoka wajibu wao kwa kushauri kwamba siku moja tutaingilia kati. Wanapaswa kutafuta suluhisho wenyewe.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isaac Gamba