Kitisho cha 'vita vya kiraia' Yemen
24 Septemba 2014Katika hotuba aliyoitoa kupitia njia ya televisheni usiku wa kuamkia leo, Rais Hadi ametoa wito wa ushirikiano kati ya serikali yake na chama cha Wasunni cha Al-Islah, ambacho amekuwa akikabiliana nacho kwa miezi kadhaa.
Kabla ya hotuba yake mapema jana, mamia ya waapiganaji waasi walishika doria kwenye vizuizi vya barabara inayoelekea uwanja wa ndege, huku wengine wakifanya ulinzi katika mitaa ya mji mkuu, wakitumia magari makubwa, kama ilivyoshuhudiwa na mwandishi wa shirika la habari la AFP. Rais Hadi alisema mgogoro wa sasa unadhaminiwa na wageni:
''Kwa wahati huu nahisi njama zinazoandaliwa nje ya mipaka yetu, zikihusisha pande kadhaa. Baadhi ya pande hizo zimepoteza matumaini, na nyingine zinataka kulipiza kisasi. Zinataka kulipiza kisasi kwa nchi yetu kwanza kabla ya kuwaendea maadui wao. Tunashuhudia wenye hadaa wakizihujumu raslimali za nche.'' Alisema Rais Hadi.
Njama za kuiangusha serikali
Kwa mujibu wa rais huyo, njama hizo kutoka nje ya nchi zimeungana kuiangusha serikali yake, ambayo ameiita ya kupigiwa mfano katika mchakato wa mpito kufuatia vuguvugu la megeuzi katika ulimwengu wa Kiarabu. Yemen ni nchi pekee ya kiarabu ambako vugu vugu hilo lilimalizika kwa makubaliano ya kisiasa, ambayo yalimuondoa madarakani rais wa muda mrefu Ali Abdullah Saleh na kumweka Abrabuh Mansur Hadi.
Licha ya kwamba makundi ya waasi yanadhibiti majengo muhimu ya utawala, kama vile Bunge, makao makuu ya jeshi na benki kuu, Rais Hadi anashikilia kuwa mjii mkuu, Sanaa hautaanguka mikononi mwa waasi hao.
Enzi mpya kwa Yemen
Kwa upande mwingine kiongozi wa waasi wa kabila la Houthi amesema taifa la Yemen limeingia katika enzi mpya, yenye msingi katika ushirikiano na kuvumiliana katika juhudi za kuijenga nchi mpya. Kiongozi huyo, Abdul-Malik al-Houthi alikuwa akiwahutubia kwa njia ya vidio maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika mjini Sanaa kusherehekea ushindi.
Siku tatu zilizopita kiongozi huyo alitia saini makubaliano ya amani kati ya kundi lake na serikali ya rais Abdrabuh Mansur Hadi, kufuatia siku nne za mapigano makali katika mji mkuu wa nchi. Abdul-Malik al-Houthi alilimwagia sifa jeshi la nchi hiyo kwa kutazama wakati waasi walipokuwa wakiyakamata majengo muhimu ya utawala.
Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo Jamal Benomar amesema kushindwa kwa jeshi la nchi hiyo kusimama kidete dhidi ya waasi kunaashiria kuporomoka kwa dola la Yemen, na mwisho wa kisiasa wa kipindi cha mpito.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae
Mhariri: Mohammed Khelef