1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kitisho cha Urusi kushawishi uchaguzi wa Umoja wa Ulaya

Oumilkheir Hamidou
13 Mei 2019

Wiki mbili kabla ya uchaguzi wa bunge la Ulaya, kamishna wa masuala ya sheria wa Umoja wa Ulaya Vera Jourova ameelezea wasi wasi wake kuhusiana na kampeni ya kueneza uongo na hasa kutoka Urusi.

https://p.dw.com/p/3IOsR
Symbolbild Fake News
Picha: Imago/ZumaPress

Kampeni za kueneza uwongo zinazosimamiwa na nchi za kigeni zimelengwa kushawishi matokeo ya uchaguzi unaokuja wa bunge la ulaya. Kamishna wa Umoja wa ulaya anaeshughulikia masuala ya sheria Vera Jourova ameonya akisema tunanukuu "Hatuwezi kuachia  hila zipotowe matokeo ya uchaguzi katika nchi yoyote ile mwanachama wa Umoja wa ulaya. Sio tuu kwasababu ni jukumu letu, lakini pia kwasababu uchaguzi huu utaamua kuhusu mustakbali wa Ulaya" amesema kamishna wa masuala ya sheria ya Umoja wa ulaya katika mahojiano na mtandao wa habari wa Ujerumani-Redaktionnetzwerk Deutschland-RND.

Kwa mujibu wa Vera Jourova, kampeni zilizoandaliwa makusudi  nchi za nje ili kueneza habari za uongo zimelengwa kushawishi mgawanyiko ulioko katika jamii."Ni shida kuwagundua.Tunashuhudia wakati huu tulio nao aina ya mashindano ya silaha za digitali. Ulaya inabidi iwe macho" amesisititza.

Katika mapambano dhidi ya habari za uongo Umoja wa Ulaya umeunda kikundi kilichopewa jina "StratCom" ili kufichusa habari za uongo kutoka Urusi. Kikundi hicho kinapitia na kunatathmini yaliyoandikwa katika vyombo vya habari vya Urusi sawa na habari zilizopotoshwa kutoka vyanzo vyengine vya habari na kuchapisha hadharani walichokigundua.

Mshika bendera  wa  orodha ya chama cha kihafidhina barani Ulaya katika uchaguzi wa bunge la Ulaya Manfred Weber wa Ujerumani
Mshika bendera wa orodha ya chama cha kihafidhina barani Ulaya katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, Manfred Weber wa UjerumaniPicha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Kamepni za habari za uongo zinailenga Ujerumani

Gazeti la Marekani la New York Times liliripoti kwamba vyanzo kadhaa vyenye mafungamano na Urusi au makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia vimekuwa vikieneza habari za uongo na zinazochochea mgawanyiko katika jamii mnamo wakati huu wa maandalizi ya uchagzuzi wa bunge la Ulaya.

Nchini Ujerumani, gazeti hilo la New York Times limesema vyanzo hivyo vinashirikiana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Chaguo Mbadala kwa ajili ya Ujerumani AfD sawa na kile cha siasa kali za mrengo wa kushoto Antifa kwa lengo la kusababisha mtengano. Wataalam walionukuliwa katika ripoti ya New York Times wamesema kampeni hii inalingana kwa kila hali na ile ya UIrusi katika kushawishi matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Marekani mwaka 2016.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Lithuania Linas Linkevicius ametoa wito watu wawe macho kuelekea uchaguzi wa bunge la ulaya anaoutaja kuwa "mtihani mkubwa kwa Umoja wa ulaya."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/DW

Mhariri: Iddi Ssessanga