Kiswahili "Stammtisch" Berlin
Watu wanaokutana kuzungumza Kiswahili Berlin
Waliokutana kwenye Kiswahili Stammtisch Berlin
Stammtisch ni neno la Kijerumani linalojumuisha maneno mawili tofauti "Stamm" ambalo maana yake ni kabila na "Tisch" ambalo maana yake ni meza. Kwa maana ya moja kwa moja ni kabila la mezani. Lakini kimsingi ni meza ya mjadala ambayo huwakutanisha watu mara kwa mara kuzungumzia au kufanya kitu wanachokipenda. Hawa ni wana Kiswahili Stammtisch hukutana mara moja kwa mwezi kuzungumza Kiswahili
Irene Günther
Mwanzilishi wa kikundi cha kiswahili Stammtisch Berlin. Alikaa Tanzania kwa mwaka mmoja na kufanya kazi ya kujitolea katika shule ya awali na shule ya msingi. Alirudi Ujerumani mjini Erlangen na kuwa anakutana na watu wanaozungumza Kiswahili kwenye Stammstisch ili kuendelea kuzungumza Kiswahili Ujerumani. Alipohamia Berlin aliamua kuanzisha Stammtisch na mwenzake Emmanuel Mtingwa Kutoka Tanzania.
Emmanuel Mtingwa
Anatokea Tanzania na ni mwanzilishi mwenza wa Kiswahili Stammtisch. Anasomea shahada ya Uzamili katika biashara mjini Berlin. Alianzisha Kiswahili Stammtisch pamoja na Irene Günther ili kuendelea kuongea lugha yake ya asili na kutengamana na Wajerumani wanaojifunza na kuzungumza Kiswahili.
Faith Kazinja Sandke
Anatokea Tanzania na alihamia Ujerumani mwaka 2014. Alisoma shahada ya Uzamili katika Uchumi jijini Berlin na sasa anafanya kazi na kuishi Berlin. Anaona Stammtisch ni sehemu nzuri ya kukutana na watu wa nyumbani na kuongea Kiswahili, lakini pia watu mashuhuri wa Ujerumani wanaopenda tamaduni za Afrika Mashariki.
Thomas Gitonga Kalunge
Anatokea Kenya na ni mshauri mwelekezi wa maswala ya biashara. Anapenda kuja kwenye Kiswahili Stammtisch kuongea na kujifunza zaidi Kiswahili. Pia anaona Stammtisch itampa motisha ya yeye kuzungumza Kiswahili na mtoto wake ambaye amezaliwa hapa Ujerumani.
Imani Moza
Anatokea Burundi na amekuja Kiswahili Stammtisch na mwanawe wa umri wa miezi mitatu. Anaona hiyo ni sehemu ambapo mtoto wake ataweza kusikia Kiswahili na kukizungumza licha ya kuzaliwa Ujerumani. Kwa mwanawe kuzungumza Kiswahili ni jambo la muhimu sana.
Hasheem Abdirashid
Anatokea Somalia ila wazazi wake wanatokea Kenya. Ni mwanafunzi wa shahada ya uzamivu mjini Potsdam. Anapenda kuja kwenye Kiswahili Stammtisch kwa ajili ya kukikuza Kiswahili chake na kujifunza kutoka kwa wengine wanaotoka Afrika Mashariki.
Asad Schwarz-Msesilamba
Ni mwigizaji na mzaliwa wa Berlin. Alioa mtanzania na ana ndugu zake kutoka Tanzania. Anaona Stammtisch ni sehemu ambayo inamwezesha kumkutanisha na watanzania waishio hapa Ujerumani pia. Hii inamsaidia kuendeleza mahusiano na Tanzania. Pembeni yake ni Msomali Hasheem Abdirashid.
Said Simba
Anatokea Zanzibar, Tanzania. Anaishi Ujerumani kwa miaka mitatu na nusu sasa. Anaishi na familia yake na kufanya kazi Berlin. Anatatajia kutafuta nafasi ya kujiendeleza kusomea masomo ya Sayansi ya Kompyuta. Anapenda kuja Stammtisch kuzungumza lugha yake ya asili na kukutana na Wajerumani ambao mara nyingi alishakutana nao Zanzibar.