Kishindo cha Makubaliano kati ya Canada na Umoja wa Ulaya
24 Oktoba 2016
Tuanze lakini na kishindo kinachowakabili viongozi wa Umoja wa Ulaya baada ya jimbo dogo la Ubeligiji kupinga kuidhinisha makubaliano ya biashara huru pamoja na Canada. Gazeti la "Freie Presse" la mjini Chemnitz linaandika:"Kwanini Wallonie ndio kwanza wanaanza kupinga? Majadiliano ya biashara huru pamoja na Canada-Ceta yameanza tangu zaidi ya miaka saba iliyopita. Kwa siri au uzembe wa aina gani yamekuwa yakifanyika? Huo ni mchezo mbaya wa kisiasa-unakiuka masilahi ya raia na majimbo. Mchezo huo unabidi ukome haraka. Kishindo cha Namur kimesababishwa bila ya shaka na siasa ya ndani. Idadi kubwa ya wakaazi wa Wallonie-eneo la viwanda lililokuwa zamani likinawiri-wanahisi wameondolewa patupu na utandawazi. Hali hiyo inapalilia hisia za kizalendo inazokabiliana nazo serikali ya chama cha Social Democratic. Matatizo mara nyingi hutupiwa jukumu Umoja wa Ulaya mjini Brussels ambao kwa upande wake hauna njia ya kushindana na tabia za watu kujipendelea.
Hisia za kujipendelea katika Umoja wa Ulaya
Kishindo cha Ceta sio pekee kinachouathiri Umoja wa Ulaya, linaandika gazeti la "Neue Osnabrücker": "Ni Picha ya kusikitisha hii ya Umoja wa Ulaya! Waingereza wanaupa kisogo Umoja wa Ulaya, mzozo wa wakimbizi umesababisha mfarakano miongoni mwa wanachama wake na sasa unazuka mvutano kuhusu makubaliano ya biashara huru-Ceta. Hisia za kujipendelea na masilahi ya nchi moja moja ndio mambo yanayotawala zaidi barani Ulaya. Hata wakifanikiwa kutia saini makubaliano hayo pamoja na Canada, bado lakini itasalia nuksi; Umoja wa Ulaya hauna nguvu za kutosha za kujadiliana. Ni suala la miundo mbinu. Bunge la Ulaya, pamoja na wabunge wake waliochaguliwa kwa njia za kidemokrasi, lina maana gani ikiwa hatimae bunge la jimbo ndilo lenye usemi wa mwisho katika suala la makubaliano ya Ceta? Jambo kama hilo halistahili kamwe kutokea. Anaepigania kuwepo Umoja wa Ulaya anabidi pia azitambue taasisi zake."
UChaguzi mkuu wa Mwakani Ujerumani
Mada yetu ya mwisho magazetini inatuwama katika maandalizi ya vyama vya kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Gazeti la "Der neue Tag" linamulika yanayoendelea miongoni mwa vyama ndugu vya Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union-CSU na kuandika: "Mtu anaweza kusema kwamba matamshi ya Manfred Weber kuelekea Angela Merkel yanafuata mkondo mpya wa Horst Seehofer anaeonyesha kutuma risala za suluhu kwa kansela. Lakini kwa bahati mbaya, hakuna anaweza kuashiria kwa uhakiki wakati gani waziri mkuu huyo wa jimbo la Bavaria atabadilisha maoni yake. Ndio maana lingekuwa jambo la maana kama kansela angeharakisha kutamka kama atapigania au la wadhifa wa kansela uchaguzi mkuu utakapoitishwa mwakani. Kwa namna hiyo tu ndipo atakapoweza kuwakusanya wafuasi wa vyama ndugu katika jimbo la Bavaria na kuwa nyuma yake.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlanmadspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga