Kipi kimembakisha Merkel madarakani muda mrefu?
13 Septemba 2017"Nikiangalia ni vituo vingapi vya nishati ya nyuklia vinajengwa duniani kote," kansela amesema alisema mwaka 2008, "itakuwa ni aibu kubwa iwapo tutaondoka kutoka sekta hii."
Lakini hicho ndio alichofanya haswa Angela MerkeL mwaka 2011. Kutokana na maafa ya Fukushima, alibadilika haraka na kutaka kufikishwa mwisho wa nishati ya nyuklia nchini Ujerumani.
Hili lilikuwa suala la msingi kwa chama cha Kijani kwa miongo kadhaa. Kinyume na matamshi yake ya hapo awali, Merkel , ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fizikia, alisema wakati huo: "Hatari ya nishati ya atomic haiwezi kudhibitiwa kwa usalama."
Katika wakati kama huo , kutumikia jeshi kwa mujibu wa sheria kulifikishwa mwisho, licha ya chama chake cha kihafidhina cha Christian Democratic Union (CDU) kutoridhia maamuzi hayo. Vijana wengi wa Ujerumani wanapendelea kutumikia jeshi, hata hivyo, ni msimamo ambao Merkel hakuufumbua macho. Kutokana na hisia mchanganyiko za Wajerumani kuhusiana na mada hiyo, uandikishwaji jeshini kwa mujibu wa sheria ulisitishwa tu badala ya kuondolewa kabisa.
Kwa mshangao wa wahafidhina wengi wenye msimamo mkali katika chama chake cha kihafidhina cha CDU, Merkel amekielekeza chama chake katika sera za siasa za wastani wakati linapokuja suala la sera za familia. Msimamo wa asili wa Christian Democrats wa "baba analeta nyumbani mkate na mama anauweka mezani " ulitupiliwa mbali baada ya uamuzi wa kutoa elimu kamili kabla ya watoto hawajaanza shule wakiwa na umri wa miaka mitatu na chini ya hapo, na mtazamo mpya kabisa wa hali halisi ya biashara na jamii.
Chama cha mrengo wa kushoto kimekuwa kikiongoza mabadiliko haya, lakini walikuwa ni wahafidhina ambao uungaji wao mkono ulisukuma sera hiyo kupita katika msitari.
Suala hili pengine zaidi ya mengine , linaakisi unyumbulifu wa kisiasa wa Merkel. Mapema majira ya joto , uchunguzi wa maoni uliotolewa na kituo cha taifa cha televisheni cha ZDF ulionesha kwamba asilimia 73 ya Wajerumani na asilimia 64 ya wapiga kura wa chama cha CDU, wanapendelea kuwapatia mashoga haki ya kuoana kama watu wengine wanaopendelea kuoana kati ya mke na mume.
Merkel alikuwa kila mara dhidi ya suala hilo, licha ya vyama vingine , ikiwa ni pamoja na chama kinachounda serikali ya mseto pamoja na chama cha CDU, chama cha Social Democratic (SPD), na kile cha kijani wakifanya suala hilo kuwa sharti la kwanza kwa kuunda muungano wa serikali baada ya uchaguzi mkuu wa hapo Septemba 24.
Merkel alibadili msimamo wake kiasi siku chache baadaye, na kuruhusu wabunge kupiga kura kwa mapenzi yao, badala ya kufuata msimamo wa chama.
Usawa wa ndoa ulipitishwa Juni 30. Merkel alipiga kura kupinga mswada huo , na kujiwekea nafasi ya uwezo wakati huo huo kuliondoa suala hilo kutoka katika uchaguzi ujao, na hatimaye mazungumzo ya kuunda serikali, wakati bado akikihakikishia chama chake cha kihafidhina kwamba hajasalim amri kwa msimamo wake wa asili.
Mwandishi: Volker Wagener / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Yusuf, Saumu