1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipchoge aweka rekodi mpya ya dunia ya Marathon

Daniel Gakuba
16 Septemba 2018

Mwanariadha wa Kenya Eliud Kipchoge ameweka rekodi mpya ya mbio za Marathon kwa kumaliza mbio za mjini Berlin katika muda wa saa 2, dakika 1 na sekunde 39. Mkenya mwingine, Gladys Cherono ameshinda upande wa wanawake.

https://p.dw.com/p/34wXg
45. Berlin Marathon 2018 Neuer Weltrekord Eliud Kipchoge
Eliud Kipchoge kwenye mstari wa kumaliza mbio za Marathon mjini Berlin (16.09.2018)Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hitij

Kwa muda huo, Kipchoge ameivunja rekodi iliyowekwa na Mkenya Mwingine Dennis Kimetto pia mjini Berlin mwaka 2014, kwa kumaliza mbio hizo kwa muda wa masaa 2, dakika 2 na sekunde 57.

Kwa maana hiyo, Kipchoge mwenye umri wa miaka 33 amepunguza rekodi iliyokuwepo kwa dakika 1 na sekunde 18, punguzo kubwa kwa rekodi iliyokuwepo, ikizidiwa tu na ile ya mwaka 1967 pale Derek Clayton aliyoivunja rekodi ya wakati huo kwa muda wa dakika 2 na sekunde 23.

''Sina maneno ya kutosha kuelezea siku ya leo'', amesema Kipchoge kwa tabasamu baada ya ushindi wa leo, na kuongezea kuwa amejawa na furaha kwa kuweka rekodi mpya ya dunia. 

Berlin Deutschland 16 09 2018 Eluid Kipchoge Kenia nach dem Start beim Berlin Marathon 2018 *
Kipchoge amewaponyoka wenzake tangu mapemaPicha: Imago/S. Wells

''Wanasema unaweza ukakosa mara mbili, lakini sio mara tatu, kwa hiyo nataka kuwashukuru wote walionisaidia'', amemalizia mwanariadha huyo, ambaye pia alipata medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya mjini Rio de Janeiro mwaka 2016.

Hakupata ushindani mkubwa

Kipchoge ameshinda mbio za leo bila upinzani mkubwa, kwani ameanza kwa kasi na kumwacha mbali kabisa Wilson Kipsang, mkenya mwenzake ambaye amejikuta akimaliza katika nafasi ya tatu. Nafasi ya pili pia imechukuliwa na Mkenya Amos Kipruto.

Rekodi nne za dunia za mwisho katika mbio za Marathon zimekuwa zikipokezanwa na Wakenya; wa kwanza akiwa Patrick Makau

(2:03:38) mwaka 2011, Wilson Kipsang (2:03:23) mwaka 2013, Dennis Kimetto (2:02:57) mwaka 2014, na sasa Eliud Kipchoge mwaka huu wa 2018.

Deutschland Berlin Marathon Siegerin Gladys Cherono Kiprono
Gladys CheronoPicha: Reuters/M. Dalder

Kwa upande wa wanawake pia Kenya imetamba, mshindi akiwa Gladys Cherono alizikamilisha mbio za leo mjini Berlin kwa muda wa masaa 2, dakika 18 na sekunde 10, akiwatangulia Waethiopia Ruti Aga na Tirunesh Dibaba ambaye alikuwa akipigiwa upatu kushinda.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe,reuters

Mhariri: Zainab Aziz