1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kipchoge aweka historia katika mbio za marathon

14 Oktoba 2019

Mkenya Eliud Kipchoge amesema anahitaji muda wa kutulia kimwili na kiakili baada ya kuwa mtu wa kwanza kukimbia mbio za marathon chini ya saa mbili katika jaribio lililofadhiliwa na kampuni ya kemikali ya INEOS

https://p.dw.com/p/3RG61
Österreich Sport l Marathon Wien - Marathonstar Eliud Kipchoge - Ziel
Picha: Reuters/L. Foeger

Ilikuwa ni wikiendi njema sio tu kwa Kenya, bali Afrika na hata ulimwengu kwa jumla wakati historia iliandikwa mjini Vienna, Austria. Mkenya Eliud Kipchoge amesema anahitaji muda wa kutulia kimwili na kiakili baada ya kuwa mtu wa kwanza kukimbia mbio za matrathon chini ya saa mbili. Kipchoge amesema hajaamua kama atatetea taji lake katika mashindano yajayo ya Olimpiki mjini Tokyo.

Bingwa huyo anayeshikilia rekodi ya dunia alitumia muda wa saa moja, dakika 59 na sekunde 40 katika jaribio lililopangwa na kampuni ya kemikali ya Uingereza INEOS. Akijibu maswali kwenye ukurasa wake wa Facebook, Kipchoge mwenye umri wa miaka 34 alisema kwa sasa anataka kurejesha nguvu mwilini

Nitachukua wiki tatu za kupata mapumziko ya kutosha. Kwa sasa nashughulika tu na kuurejesha mwili katika hali nzuri na siwazi kuhusu changamoto nyingine yoyote kwa sasa

Kipchoge anaamini ushindi wake wa Vienna, utakihimiza kizazi kijacho cha wanariadha kufanya bidii na kuvunja vizingiti nchini mwake.

Nataraji kuwa na ninauonyesha ulimwengu kuwa hakuna mtu aliye na ukomo, na wanaweza kukimbia chini ya saa mbili. Natarajia wanariadha wengi kufanya mazoezi vizuri na kukimbia chini ya saa mbili kama nilivyofanya leo.

Tukio hilo la kihistoria liliibua shangwe na vifijo kote kote Kenya kuanzia Nairobi hadi Eldoret – mji anakotokea, ambapo kila mmoja alifuatilia moja kwa moja. Jamaa zake katika Kaunti ya Nandi pia walijumuika pamoja ili kuwa sehemu ya historia.