1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi wa Wapalastina, Yasser Arafat, yu mgonjwa sana

28 Oktoba 2004

Madaktari wa Kipalastina pamoja na wale wa kutokea Tunisia na Jordaan wamependekeza kiongozi wa Kipalastina, Yasser Arafat, aliye mgonjwa sana ahamishiwe hospitalini kutoka makao yake makuu ya huko Ramallah, lakini uamuzi utatolewa huenda baadae leo. Pia Israel imesema itamruhusu Arafat asafiri kwenda kokote kupata matibabu, ikiwa ni alama ya kuonesha huruma ya kiutu.

https://p.dw.com/p/CEHR
Kiongozi wa Wapalastina, Yasser Arafat
Kiongozi wa Wapalastina, Yasser ArafatPicha: AP

Wapalastina wanasema kiongozi wao amekuwa na maumivu ya tumbo tangu wiki iliopita, wengine wakisema ameshikwa tu na mafua makali. Lakini hali yake ya afya ilizidi kuwa mbaya jana na kuna maafisa waliosema kuna nyakati hupoteza fahamu- jambo ambalo lilikanushwa baadae- japokua leo aliweza kula, kuzungumza na pia kusali. Afisa mmoja alisema Arafat yuko katika hali mbaya, na humwita mkewe. Kwamba Arafat yuko katika hali mbaya kulielezewa pia na waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Silvan Shalom, japokuwa yeye alitahadharisha kwamba ni mapema mno kuusoma uwasifu wake. Mkewe, Bibi Suha, na binti yao, wameondoka Tunis leo kukimbilia kuweko karibu na mgonjwa huyo. Mfanya biashara ambaye yu karibu na Arafat, Munib al-Masri, aliwaambia waandishi wa habari baada ya kukutana naye leo kwamb kiongozi huyo wa Wapalastina anataka kuwaambia wananchi wa Kipalastina na watu wa dunia nzima kwamba yu mzima na hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu yake.

Yasser Arafat amekuwa akiugua magonjwa kadhaa, na amekuwa akitetemeka kidogo, akidhaniwa ana ule ugonjwa wa Parkinson, kama ule anaouguwa Popa Yohana Paul wa Pili au yule bingwa maarufu wa ndiondi, Mohammed Ali.

Viongozi wa Kipalastina wanapanga kuwa na mkutano leo juu ya mzozo huu, wakati waziri mkuu wa Wapalastina, Ahmed Qurei, ameshazungumza kwa simu na mwenzake wa Israel, Ariel Sharon, ambaye aliahidi kufanya kila kitu cha lazima kwa ajili ya afya ya Arafat. Raanan Gissin, msemaji wa waziri mkuu Ariel Sharon, alisema huko Jerusalem kwamba Israel itamruhusu Arafat asafari kwenda kokote kwa ajili ya kupata matibabu, hii ikiwa ni alama ya huruma ya kiutu. Alipoulizwa ikiwa Israel itamruhusu Arafat arejee Ukingo wa Magharibi baada ya kuondoka, Bwana Gissin alisema ikiwa madaktari watasema anahitaji kurejea baada ya kupata matibabu, basi Israel haitaweka vizuwizi vyovyote juu ya jambo hilo. Israel hapo awali ilisema haingetoa uhakikisho juu ya kurejea Arafat ikiwa ataondoka Ramallah, lakini Ariel Sharon amebadilisha msimamo baada ya kuzungumza kwa simu jana usiku na waziri mkuu wa Wapalastina, Ahmed Qurei. Israel mara kadhaa ilitishia itamfukuza Arafat kutoka Ukingo wa Magharibi au hata kumuuwa, na ikashauri kwamba pindi ataondoka kutoka maeneo ya Wapalastina, basi hatoruhusiwa kurejea.

Pindi Yasser Arafat atakufa, basi spika wa bunge la Wapalastina, Rawhi Fattouh, atachukuwa nafasi yake kama rais wa Mamlaka ya Serekali ya Wapalastina kwa siku 60, wakati ambapo uchaguzi utabidi ufanye. Nani atachukuwa nyadhifa zake mbili nyingine, kama kiongozi wa Chama cha Ukombozi, PLO, na vuguvugu la Chama cha al-Fatah, bado haijulikani. Pia kuna wasiwasi, pindi atafariki, juu ya mpango wa waziri mkuu wa Israel, Ariel Sharon, wa kuondosha majeshi ya nchi yake kutoka Ukanda wa Gaza na baadhi ya maeneo katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, hatua iliozusha mzozo wa kisiasa katika dola ya kiyahudi ya Israel. Waziri wa mambo ya kigeni wa Israel, Silvan Shalom, alizusha uwezekano wa kuanzisha mazungumzo mepya na Wapalastina pindi Arafat atafariki dunia. Alisema wao wamekuwa maisha tayari kuzungumza na uongozi wowote wa Kipalastina ambao una nia ya kuzuwia damu kumwagika.

Wenyewe Wapalastina hawaridhiki namna wanavofichwa juu ya habari ya kuuguwa kiongozi wao. Wana wasiwasi kifo chake kitazusha michafuko mingine. Pia Wa-Israeli wana wasi kwamba baada ya Arafat, asije kiongozi mwengine wa Kipalastina aliye na siasa kali zaidi kuliko za Arafat, au kutoka makundi ya Kiislamu yenye siasa kali, kama vile kundi la Hamas. Kuna Wapalastina wengine wanaosema bora Arafat afariki dunia baada ya miezi hivi kupita, sio kwamba wanamtaka aweko kwa muda mrefu zaidi, lakini wanataka taratibu za kisiasa za nyadhifa zake kukamatwa na nani zinahakikishwa ili kuepusha michafuko.

Ziara iliopangwa kufanywa na waziri wa mambo ya kigeni wa utawala wa Wapalastina, Nabil Shaath, huko Mosko sasa imevunjwa. Bwana Shaath alipangiwa akutane na waziri wa mambo ya kigeni wa Russia, Sergei Lavrov, hapo kesho.

Miraji Othman